April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Profesa Ndalichako atoa vyerehani 10

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikabidhi fedha taslimu kiasi cha Sh. 500,000 kwa mmoja wa wanafunzi wa VETA Mpanda aliowapati cherehani kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuwawezesha kuanza kushona ili waweze kujiingizia kipato.

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa vyerehani 10 kwa wanafunzi waliohitimu​ mafunzo ya ushonaji kutoka Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi​ (VETA) Mpanda​ wanaotoka katika mazingira magumu.
​
Akizungumza katika halfa ya kukabidhi vyereheni hivyo Mkoani Katavi, Profesa Ndalichako amesema, ahadi hiyo aliitoa​ mwaka 2018 baada ya kuwakuta vijana wadogo wamemaliza masomo ya darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari​ na kujiunga na mafunzo ya ushonaji katika chuo hicho kupitia msaada wa kanisa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa VETA Mpanda wanaotoka katika mazingira magumu mara baada ya kuwakabidhi cherehani alizoahidi kuwapatia.

​“Mwaka juzi nilifika katika chuo hiki na kuwakuta hawa vijana wawili wadogo wakiwa katika mafunzo ya ushonaji na nilipozungumza nao niligundua kuwa wametoka katika mazingira magumu, hivyo kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari, ndipo nilipowaahidi kuwapatia vyerehani watakapomaliza ili viwawezeshe kujiajiri,” amesema Profesa Ndalichako.

Hata hivyo, Profesa Ndalichako amemuagiza, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Mpanda kuona namna ya kuwapatia nafasi ya kuendelea na ngazi nyingine ya mafunzo watoto hao​ ili waweze kuwa mahiri zaidi katika ushonaji .

Mkuu wa Chuo hicho, Elisha amemshukuru waziri kwa kutimiza ahadi aliyoitoa mwaka 2018 kwani inakwenda kuinua watoto wanaotoka katika familia masikini na kuahidi kuwasimamia ili cherehani hizo ziwe na manufaa kwa watoto wenyewe na familia zao.
​
Mmoja wa wanafunzi waliopatiwa cherehani, Gift Giles amemshukuru Waziri kwa kuwapatia cherehani hizo ambazo zinakwenda kubadili maisha yao.