April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makonda aagiza Takukuru kufanya Uchunguzi wa Bilioni 33 za Mikopo ya Manispaa

Na Penina Malundo, Timesmajira Online

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameitaka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru ) kuanza mara moja uchunguzi wa Shilingi Bilioni 33 za mikopo ya asilimia 10 iliyotengwa kwa ajili ya makundi ya Vijana, Kinamama na Walemavu katika Halmashauri kama zimewafikia walengwa.

Agizo hilo amelitoa wakati wa Mwendelezo wa ziara ya Kukabidhi Miradi kwa Chama cha Mapinduzi Jimbo la Ubungo.

Amesema, Takukuru inatakiwa kuhakikisha kabla ya Julai 20, mwaka huu inampatia mchanganua wa namna pesa hizo zilivyotumika kwa kuwa Rais Magufuli aliondoa riba kwenye mkopo huo ili kuyawezesha kiuchumi makundi hayo.

Hata hivyo katika ziara yake, Makonda amekabidhi miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 559.6 kwa Chama cha Mapinduzi kwa Jimbo la Ubungo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho.

Miongoni mwa Miradi aliyokabidhi ni Daraja la Juu Ubungo lenye thamani ya Bilioni 299, Upanuzi wa Mto Ng’ombe Bilioni 32.5, Ujenzi wa Barabara ya Shekilango na Viunga vyake Bilioni 26 na Ujenzi Wa jengo la Wodi ya Wagonjwa na Upasuaji Hospital ya Palestina.

Miradi mingine aliyokabidhi ni Ujenzi miundombinu ya Madarasa Name , Matundu 12 ya Vyoo na uzio kwenye Shule ya Ubungo plaza pamoja na kukagua Vikundi 20 vya wajasiriamali waliokopeshwa fedha kupitia asilimia 10 za Manispaa.