April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi

Siri za Tanzania kuwa na uchumi wa kati hizi hapa

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, ametaja siri ambazo zimeiwezesha Benki ya Dunia (WB) kuitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani za uchumi wa kipato cha kati.

Tanzania inakuwa ya pili baada ya Kenya katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, baada ya ukuaji wa uchumi unaosukuma pato la mwananchi kukua (Per capita GNI) mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Dkt. Abbasi alisema kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025 katika ukurasa wa pili, kipengele 1.2 , Uchumi wa kipato cha kati umehusishwa na kuwa na nchi ambayo umaskini unapungua, uchumi imara unaojengwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani unaimarika na wananchi wanapata maendeleo”.

Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa uchumi wa kipato cha kati umegawanyika katika madaraja mawili daraja la chini ambapo ni kuanzia dola za Kimarekani 1,036 hadi 4,045 na daraja la juu ni dola 4046 hadi 12,535 na mwaka huu Tanzania imepanda daraja kuwa uchumi wa kipato cha kati daraja la chini, pamoja na nchi za Algeria na Benin.

Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua siri 10 zilizoisaidia Tanzania kutajwa kufikia daraja la uchumi wa kipato cha kati na Benki ya Dunia Julai 1, 2020 kuwa ni nchi yenye amani na utulivu, na hivyo ni msingi muhimu nyuma ya mafanikio ya nchi ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kipato cha kati.

Alisema bila amani hakuna kufanyakazi, hakuna kuzalisha na hakuna kuongeza kipato. “Na hivyo viongozi, wanahabari na wananchi kwa ujumla kuwekeza akili zao katika kuimarisha amani iliyopo na kukataa chokochoko zozote zile zinazoweza kuharibu misingi ya maendeleo,”alisema.

Siri ya pili ni mipango thabiti ya maendeleo, ambapo Dkt. Abbasi alisema kuwa moja ya kanuni muhimu ya kuendelea ni kuwa na mipango inayokuwekea malengo makubwa (Olympic targets).

Alisema Serikali itaendelea kuweka mipango mbalimbali ya maendeleo ya muda mrefu na mfupi, akitolea mfano mwaka 2020 Serikali ilianza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo moja ya malengo ni kufikia uchumi wa kati.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi siri ya tatu ni utekelezaji usioyumba, katika miaka 59 ya Uhuru na mitano ya Awamu ya Tano Serikali imejitahidi kusimamia eneo hilo kwa kuhakikisha mipango inayowekwa inatekelezwa kwa kina (3feet implementation).

Mitambo ya kufua umeme

Siri nyingine ni maamuzi magumu, “Moja ya mafanikio ya Serikali ya Tanzania kwa Awamu zote na sasa tumeimarisha katika Awamu ya Tano ni wakati fulani Serikali kufanya uamuzi mgumu ambao wakati fulani ulionekana kuwa ni ndoto lakini baadaye ukaleta mafanikio makubwa kwa jamii, tumepambana na wala rushwa na wahujumu uchumi, tumewekeza katika miundombinu mikubwa, tumekataa pia baadhi ya nadharia za kimagharibi kwenye utendaji wetu na utungaji wetu wa sera za maendeleo” alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, Dkt. Abbasi alitaja siri nyingine kuwa ni azma ya kujitegemea, nidhamu katika matumizi, kutekeleza miiko ya uongozi, kuwekeza kwenye miradi inayochechemsha uchumi, maendeleo ya vitu na sekta binafsi yenye tija.