April 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angellah Kairuki akizungumza na Menenjimenti ya Kiwanda cha Sukari -TPC kilichopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro (Hawapo pichani) alipotembelea kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake .

Serikali yaitaka TPC kuzalisha sukari ya viwandani

Na Dixon Busagaga – Kilimanjaro .

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia uwekezaji, Angela Kairuki,ameutaka uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, kilichopo Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kuangalia uwezekano wa kuanza uzalishaji wa Sukari ya viwandani, ili kuondoa adha ya kuagiza sukari hiyo nje ya nchini.

Afisa Mtendaji -Utawala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC-Jafary Ally akielezea jambo mbele ya Waziri Kairuki alipotembelea kiwandani hapo .

Kairuki alisema mpaka sasa hakuna mzalishaji wa sukari za viwandani nchini na kwamba serikali huagiza zaidi ya Tani 155,000,na kwamba endapo TPC wataanza uzalishaki huo, watasaidia upatikanaji wa sukari hiyo kwa urahisi.

“Niwashauri TPC, kuangalia ni namna gani,mnaweza kuzalisha sukari za viwandani, tukitambua bado hatuna mzalishaji hata mmoja hapa nchini, ambaye anazalisha sukari za viwandani,tunaagiza zaidi ya tani 155,000 za sukari hii, tunamini mkileta mitambo, mnaweza kuzalisha na kuweza kupata sukari hiyo hapa nchini”alisema Kairuki

Afisa Mtendaji -Utawala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC-Jafary Ally (Wa pili kutoka kulia) akimuongoza Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angella Kairuki kutembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho.

Mbali na hilo Kairuki amewataka wawekezaji, kuendelea kutazama fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwekeza katika nyanja mbalimbali, ili kufanikisha malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.

Alisema bado kuna mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali nchini, na bidhaa nyingine zinaagizwa nje ya nchi, hivyo ipo haja kwa wawekezaji kujitokeza na kuwekeza katika nyanja mbalimbali, hatua ambayo itapanua wigo wa ajira kwa watanzania na hata kuinua pato la taifa.

Sehemu ya Kiwanda cha Sukari cha TPC
Waziri Kairuki akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi a kiwanda cha Sukari cha TPC namna ambavyo machine ya kuzalisha umeme kiwandani hapo inafanya kazi .

“Mahitaji bado ni makubwa nchini, kuna changamoto ya chupa za kioo,Chupa za Plastiki na bidhaa nyingi tunaagiza nje, sasa angalieni, mkiona kuna fursa, serikali tupo tayari kutoa ushirikiano, ili muweze kupanua wigo wa uwekezaji”alisema Kairuki.

Akizungumza Ofisa mtendaji utawala katika kiwanda cha TPC, Jaffari Ally,alisema mpaka sasa kiwanda hicho kina sukari zaidi ya tani 3,300 ambazo zipo kwenye Ghala, na kuwatoa hofu watanzania, kuwa hakuna tena upungufu wa sukari nchini.

“Tuwatake wasambazaji wakubwa na wauzaji wa rejareja wa sukari nchini, kuacha kuwalangua wananchi na kuhakikisha wanauza sukari kwa bei ya awali ya kabla ya kufungwa kwa msimu, maana kwa sasa sukari inayouzwa inazalishwa hapa nchini na hakuna inayoagizwa nje ya nchi”alisema.

Waziri Kairuki akitizama namna ambavyo sukari inawekwa kwenye mifuko kabla ya kwenda kwa mtumiaji wa mwisho .
Sehemu ya Mabehewa yanayotumika kusafirisha Miwa kutoka mashambani na kuifikisha katika eneo la kiwanda .