May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa 

Na Mwandishi wetu,Timesmajira 

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA)imekamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Mpanda na Pemba ikiwa ni uboreshaji wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa sekta ndogo ya usafiri wa anga.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo jana wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/27 jijini Dodoma, ambapo amesema Serikali kupitia Mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini sambamba na kuhakikisha huduma hizo zinadhibitiwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo usafiri wa anga.

Amesema kuwa TMA imeendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa lengo la kuongeza usalama, ufanisi na uhakika wa shughuli za usafiri pamoja na sekta nyingine zinazotegemea taarifa za hali ya hewa.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya hali ya hewa ili kuimarisha uwezo wa utoaji wa taarifa sahihi na za wakati, hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza usalama katika sekta ya usafiri na shughuli nyingine za kiuchumi nchini.

” Serikali kupitia TMA imeendelea na utoaji wa huduma za hali ya hewa, pamoja na kudhibiti na kuratibu shughuli zote zinazohusiana na hali ya hewa nchini na kutekeleza majukumu mengine yakiwemo kufanya tafiti za kisayansi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na kubadilishana taarifa za hali ya hewa kupitia mtandao wa mawasiliano wa dunia wa Global Telecommunication System (GTS) kwa kuzingatia makubaliano ya kimataifa.

”Kutokana na umahiri wa TMA kimataifa, taasisi hii imeendelea kuiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa na hivyo kuendelea kuchangia katika uimarishaji wa mifumo ya tahadhari za mapema dhidi ya majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa,”amesema Prof. Mbawara