Na. Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango Dkt. Tausi Kida ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Dkt. Jim Yonazi kilicholenga kujadili utendaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka -BRT leo 04 Agosti, 2026 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Tausi ameongoza kikao hicho kilichoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa ya timu ya wataalam kuhusu utendaji wa Mradi huo ambapo imeelezwa kuwa lengo la Mradi huo ni kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika Mkoa wa Dar es salaam kwa kuboresha huduma ya usafiri kwa Jamii.
Kikao hicho kilijumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Tume ya Taifa ya Mipango, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi, WIzara ya Uchukuzi, Msajili wa Hazina, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).
Aidha, Dkt. Tausi ametumia kikao hicho kuwakumbusha watendaji kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi huku akieleza lengo la Serikali la kuendelea kuwapatia wakazi wa jiji la Dar es salaam usafiri bora, wa haraka na salama na kuendelea kupunguza msongamano wa magari ili kuokoa muda wa safari na kuboresha usalama barabarani.
“Mradi huu utumike kama ilivyokusudiwa na kuendelea kujiratibu vyema ili kuendelea kutoa huduma bora za usafiri kwa wananchi,” alisema Dkt. Tausi

More Stories
Mwanasheria Mkuu wa Serikali awataka TPBA kuwa wabunifu
SCADA waimarisha udhibiti wa mafuta nchini
Vijana wa BBT watafuta fursa TADB