August 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PDPC yaanza ukaguzi uzingatiaji Sheria

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online


TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeanza ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, kwa taasisi, mashirika, wafanyabiashara na wadau wanaokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kuanza kwa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema ukaguzi huo unalenga kuhakikisha taarifa binafsi za watumiaji wa huduma mbalimbali zinakusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria.


Amesema Tume ilitoa muda wa kutosha kwa taasisi, mashirika, wafanyabiashara na wadau wote wanaokusanya na kuchakata taarifa binafsi kujiandaa kwa utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.


Kwa mujibu wa Dkt. Mkilia, ukaguzi huo unahusisha kuhakiki iwapo taasisi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi zimesajiliwa na Tume kwa mujibu wa Kifungu cha 14(1) na 14(2) cha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.


Aidha, Tume itahakiki usahihi wa taarifa za usajili zilizowasilishwa na wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi katika rejesta ya Tume, pamoja na utekelezaji wa majukumu ya Afisa Ulinzi wa Taarifa.


Ukaguzi pia utahusisha namna taarifa binafsi zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa, pamoja na hatua zinazochukuliwa na taasisi kuhakikisha usalama wa taarifa hizo dhidi ya upotevu, uteketezaji, ubadilishaji, upatikanaji au uchakataji usioidhinishwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 27(1) cha sheria hiyo.


Tume pia itahakiki taratibu za usafirishaji wa taarifa binafsi nje ya nchi kwa kuzingatia Kifungu cha 31 na 32 cha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.


Dkt. Mkilia amesema ukaguzi huo unaweza kuambatana na hatua za kisheria, ikiwemo utoaji wa adhabu na faini kwa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi ambao watabainika kutokuzingatia matakwa ya sheria.


Ametoa wito kwa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi kuhakikisha wamesajiliwa katika rejesta ya Tume, wanazingatia haki za wahusika wa taarifa, na wanakusanya pamoja na kuchakata taarifa hizo kwa madhumuni halali na mahususi yaliyokusudiwa.


Pia, amewataka kuhakikisha wanawasilisha Ripoti ya Uzingatiaji kila robo ya mwaka, kuzingatia Sera ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyoidhinishwa na Tume, na kuhakikisha taarifa binafsi hazisafirishwi nje ya mipaka ya nchi kinyume cha sheria.


Kwa upande wa ridhaa, Tume imewataka wakusanyaji na wachakataji kupata ridhaa ya wahusika wa taarifa kabla ya kukusanya au kuchakata taarifa zao binafsi pale ambapo sheria inahitaji ridhaa hiyo.


Tume imesema hatua inayofuata ya zoezi hilo itahusisha kutembelea taasisi na wadau wanaokusanya na kuchakata taarifa binafsi ili kujiridhisha zaidi kuhusu uzingatiaji wa matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.


Tume imesisitiza kuwa inatarajia ushirikiano kutoka kwa wadau wote ili kufanikisha zoezi hilo na kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi nchini unaimarishwa.