August 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muhimbili Mloganzila, Mwananyamala waungana kuboresha Afya

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila umetembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala, kwa lengo la kujadili maeneo ya ushirikiana na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu ili kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba Dkt. Elineema Meda amesema ushirikiano kati ya hospitali hizo ni muhimu katika kubadilishana uzoefu, ujuzi na mbinu bora za utoaji wa huduma, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi za afya kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya afya.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala Aileen Barongo amesema ziara hiyo ni fursa muhimu ya kujadili maeneo ambayo hospitali hizo zinaweza kushirikiana, pamoja na kujifunza kutoka katika uzoefu wa kila upande.

Katika ziara hiyo wametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo idara ya magonjwa ya dharura na kitengo cha uchujaji damu ( dialysis) kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.