April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman ataka ushirikiano na familia duni Z’bar

Na Haji Mtumwa, TimesMajira Online, Zanzibar

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Ili kuziondoa changamoto zinazozikabili familia duni, kunahitaji ushirikiano kati ya viongozi na jamii husika.

Othman ameyasema hayo leo katika ziara yake maalum ya kuwafariji na kuwapa pole wagonjwa, watu wasiojiweza na familia za wafiwa mbalimbali, ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kuwa zipo changamoto ambazo siyo shida kuzitatua, bali baadhi yao zinahitaji ushirikiano wa pamoja kukabiliana nazo, kutokana na jinsi zinavyozorotesha na kudhoofisha ustawi wa watu, familia na jamii kwa ujumla, hali ambayo inagusa hisia za kila mwenye huruma.

Othman ametolea mifano hali za unyonge, ufukara wa kupindukia, kuondokewa, maradhi, udhaifu na ukosefu wa kudumu wa kipato na mahitaji ya lazima, kuwa kwa sasa ni miongoni mwa changamoto zinazodhoofisha ustawi wa familia nyingi, katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Othman ametoa wito kwa jamii kuutumia vyema Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuhakikisha kunakuwepo ushirikiano wa kuwasaidia wale wasiojiweza wakiwemo wazee, wagonjwa, wajane, watoto yatima na watu wenye ulemavu, ili kutoa unafuu wa kupata huduma za msingi na ah-weni ya kimaisha.

Wakiongelea juu ya wajibu wa kuwafikia na kuwasaidia watu wenye mahitaji na wasiojiweza, hasa katika msimu huu wa funga, Mohamed Nyasa Juma wa Donge-Njia ya Mtoni, na Tatu Haji wa Bumbwini-Uwandani, pamoja na kushukuru juhudi za viongozi katika kufanikisha utoaji wa huduma na misaada kwa wananchi, wamesema wahitaji ni wengi, na wapo miongoni mwa watu hali zao ni dhaifu mno na za kukatisha tamaa, na hivyo kunahitajika kasi zaidi ya kuwakirimu.

Katika ziara hiyo, Othman ametembelea pia vijiji vya Kitope-Mkaratini, Kikobweni, Chutama, Muwange, Tazari, Mkokotoni, Mwanakombo na Langoni ambavyo ni katika Majimbo ya Mahonda, Nungwi, Chaani, Mkwajuni, Kijini, Tumbatu, Donge na Bumbwini, ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Jamii, Vyama vya Siasa, na Vikosi vya Ulinzi na Usalama wamejumuika katika ziara hiyo wakiwemo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Bimani na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu wa Chama hicho, Pavu Juma Abdalla.Â