April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

OSHA yaungwa mkono siku ya usalama na afya

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kuadhimisha Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani, ambayo kitaifa itafanyika Njombe Aprili 28 mwaka huu, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), unatarajia kuendesha Kliniki Maalumu ya Uchunguzi wa Afya.

Kliniki hiyo inayojulikana Imarisha Afya na Mama Samia itahusisha uchunguzi wa magonjwa kwa wananchi kama saratani, shikinikizo la damu, sukari, magonjwa ya wanawake, macho, mifupa na hali lishe.
Lakini pia itatoa dawa kwa wananchi watakaopima afya kwenye kliniki hiyo katika kiwanja cha Shule ya Msingi Mji Mwema, Njombe.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam.

Alikuwa akipokea msaada kutoka kampuni ya dawa ya Planet ya Dar es Salaam ambapo alitoa mwito kwa wadau kutoa msaada kwa ajili ya wananchi watakaofika kupata huduma kwenye kliniki hiyo.

Amesema mwaka huu wamekuja kivingine, na uchunguzi wa afya kutoka kwa madaktari bingwa na kutoa dawa kwa wagonjwa, kwani miaka iliyopita, walikuwa wakitoa ushauri na kupima afya pekee.

Khadija amesema maonesho hayo yatakayoanza Aprili 24 na kukamilika Aprili 29 mwaka huu, yatahusisha zaidi ya kampuni 100 na wajasiriamali, hivyo wanaamini wananchi wengi watajitokeza kupima afya na kupata ushauri na dawa.

“Katika kuadhimisha Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi, tumekuwa tukitoa mafunzo, kufanya maonesho, kutoa tuzo, misaada ya vifaa kinga na kliniki maalumu.

“Hivyo naomba wana Njombe na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi, tunashukuru sana Planet kwa kutupa dawa hizi na tunaomba wadau wenye viwanda vya dawa watusaidie,” amesema.

Mtendaji huyo wa OSHA amesema hadi sasa wana miaka mitano wakitoa huduma hiyo kupitia Programu ya Imarisha Afya na Mama Samia, na wamekuwa wakihudumia zaidi ya watu 5,000 kila mwaka na matarajio yao ni mwaka huu, kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 10,000.

Khadija amesema wanatarajia kuwa na madaktari bingwa kutoka hospitali za Muhimbili, Mirembe, Njombe, OSHA na kwingine.

Meneja Rasilimali wa Kampuni ya Dawa ya Planet, Andrew Paul amesema walitoa msaada huo, kama sehemu ya kurudisha shukurani kwa jamii, yenye mchango mkubwa wa uwepo wao.

“Hiki tulichotoa hapa OSHA, ni sehemu ya sisi kurudisha shukurani kwa jamii, ambayo imekuwa ikituunga mkono kila siku na kwamba tunaahidi kuendelea kushirikiana na wakala huyu,” amesema.

Amesema OSHA ni mdau muhimu katika shughuli zao jambo linalofanya waendelee kuimarika kila siku, katika kuhudumia wananchi.