April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 70 ya lengo yafikiwa Ilemela

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

HADI kufikia Machi 31 Machi, 2026 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani kiasi cha zaidi ya bilioni 11.5,sawa na asilimia 70 ya lengo la mwaka.

Ambapo halmshauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, iliidhinisha kukusanya kiasi cha zaidi ya bilioni 16.4,katika bajeti ya mapato ya ndani.

Hayo yameelezwa Aprili 21,2026, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,wakati akiwasilisha taarifa za utekelezaji robo ya tatu kipindi cha Januari – Machi 2025/2026,katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmshauri hiyo.

“Niombe na nitoe rai sisi na wananchi wetu,tuendelee kuwaelimisha kuhusiana na mapato haya ya halmashauri kwa sababu tunaona faida yake,fedha hizi zinarudi kwao kwa ajili ya kuboresha hali ya utoaji huduma katika maeneo yao,”amesema Ummy.

Sanjari na hayo, Ummy amesema katika kipindi cha Januari-Machi 2026,halmashauri imeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya bilioni 44.6.

“Miradi hii inatekelezwa kupitia mradi wa uendelezaji Miji na Majiji (TACTIC), Programu ya Green & smart City SASA, mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na ruzuku kutoka Serikali kuu,”amesema Ummy na kuongeza:

“Tunaendelea kutoa hizi fedha ili kutimiza yale malengo ambayo Rais anatamani yatokee,tushirikiane katika utekelezaji wa miradi hii.Madiwani tupite kwenye miradi iliyotekelezwa ili unapoona jambo haliko sawa hatua za awali inakuwa rahisi kutoa taarifa, tunachukua hatua mapema kuliko kusubiri jambo limeharibika mnafika wote mnaanza kushangaana,”.

‎Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kafiti William,ametoa wito kwa wakuu wa idara wa halmshauri hiyo kutoa ushirikiano na kusaidia ushauri wa kitaalamu ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
‎
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela, Yusuph Bujiku ameitaka serikali kushughulikia kero za wananchi kwani zinafanya wanatukanwa mitaani na kufanya chama hicho kuchukiwa.