*Akutwa ametelekezwa makaburini akiwa na michubiko usoni
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kumpata mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu na miezi kumi, ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kisheria.
Mtoto huyo ameripotiwa kupotea Aprili 18, 2026 katika Kituo cha Polisi, baada ya mama yake mzazi kudai kuwa aliibwa kwa kubebwa na mtu asiyejulikana kwa kutumia pikipiki katika eneo la Kona ya Bwiru, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Akizungumza Aprili 21,2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa,amesema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 18, 2026 majira ya saa 5:00 asubuhi mtaa wa Barabara ya Vumbi, Kona ya Bwiru.
Ambapo mama wa mtoto huyo, Neema Sesela (19), mama lishe na mkazi wa Mnyampala “B”, Kata ya Nyamanoro, alikuwa katika shughuli zake za kila siku alipogundua kuwa mtoto wake ameondolewa na mtu asiyejulikana kwa kutumia pikipiki isiyofahamika namba zake za usajili.
Baada ya tukio hilo, mama huyo alifika Kituo cha Polisi Kirumba na kutoa taarifa, ambapo uchunguzi ulianza mara moja kwa kuwahoji mashuhuda mbalimbali. Mkazi mmoja alitoa kumbukumbu za kamera za ulinzi (CCTV) zilizoonesha mwanaume akiondoka eneo la tukio akiwa amembeba mtoto huyo kwenye pikipiki, ingawa namba za usajili hazikuonekana wazi.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi lilianzisha msako wa kumtafuta mtoto huyo. Hatimaye, Aprili 20, 2026 majira ya saa 3:30 usiku, zilipatikana taarifa za kuwepo kwa mtoto wa kike aliyetelekezwa katika makaburi ya Nyasaka, wilayani Ilemela. Wasamaria wema walimuokota mtoto huyo na kumpeleka kwa mwenyekiti wa mtaa wa Nyamuge, Kata ya Nyasaka.
Polisi walifika eneo hilo na kumkuta mtoto akiwa na michubuko usoni, kisha wakampeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure kwa uchunguzi na matibabu. Wazazi wake, Neema Julius Sesela (19), mama lishe, na Mwankunja Edward (30), fundi seremala, wakazi wa Mnyampala “B”, wamemtambua mtoto huyo kuwa ni wao.
Uchunguzi wa afya ya mtoto unaendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou- Toure huku jeshi hilo linatoa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha uangalizi wa watoto ili kuhakikisha usalama wao.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT