Na Judith Ferdinand,Mwanza
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wamehoji juu ya kero ya mgao wa maji na kukatika kwa umeme maeneo mbalimbali ya halmshauri hiyo bila uwepo wa taarifa za kina, wakidai hali hiyo inaathiri shughuli za maendeleo na ustawi wa wananchi.
Hoja hizo zimeibuliwa Aprili 21, 2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani la kupokea taarifa za robo ya tatu (Januari -Machi2025/2026),kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo , wilayani Ilemela wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Pasiansi, Jonesia Kashazo,amehoji kuhusu kukatika kwa umeme bila taarifa siku za hivi karibuni,changamoto za kulipuka kwa transfoma na uwepo wa nguzo zilizotelekezwa barabarani bila kuondolewa.
“Kuna baadhi ya maeneo kama Mecco transfoma zimekuwa zikilipuka kutokana na kuzidiwa huku maeneo mengine umeme ni mdogo, tatizo ni nini?.Lakini ni lini Tanesco watasambaza nguzo katika Kata ya Kayenze, Bugogwa na Sangabuye ili nao wapate huduma ya umeme,”amesema Jonesia.
Akijibu maswali hayo, Meneja wa Tanesco Kanda ya Nyakato Wilaya ya Ilemela, Mhandisi Sarah Sangija,amekiri kuwepo kwa tatizo la kukatika kwa umeme kwa baadhi ya maeneo,huku akieleza kuwa changamoto hiyo husababishwa na hitilafu ya umeme isiyotarajiwa inayotokana na uharibifu wa miundombinu, mvua, upepo na hitilafu za ghafla katika vituo vya kupooza umeme.
”Tunaendelea kufanya ufuatiliaji na kutoa taarifa kadri inavyowezekana.Tatizo la umeme mdogo na kulipuka kwa transforma husababishwa na kuzidiwa kwa mzigo (mahitaji ya umeme kuwa makubwa), hitilafu ya kiufundi na uchakavu wa vifaa,”amesema Mhandisi Sarah.
Hata hivyo,amesema kuwa hatua zinazochukuliwa kwa sasa ni kufunga mashine mpya, kuboresha huduma, kugawa mzigo kwa kuongeza mashine, huku wakiwa tayari wamefanya maboresho katika maeneo ya Nyasaka, Bwiru, Kiseke, Bidii, Zenze, Ilalila, Nyakato na mengineyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ibungilo, David Lucas amehoji ni lini tatizo la mgao wa maji usiofuata mpangilio ambao hauna taarifa litaisha,pia alihitaji kufahamu kwanini kumekuwa na kero kwa wananchi kubambikiziwa ankara ya maji ambayo haiendeni na matumizi yao.
”Lakini sote tunakumbuka katika kikao cha Januari 29, 2026,tulitaarifiwa kuwa MWAUWASA wangepata mita 15,000 kufikia Februari, nini kinafanya wateja wapya kushindwa kuunganishiwa huduma ya maji?,”amehoji Lucas.
Akitolea ufafanuzi wa hoja hizo, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Wilaya ya Ilemela, Salum Lossindilo,amesema ni kweli kumekuwa na mgao wa maji ambao unatokana na uzalishaji mdogo, kuyumba na kukatika umeme mara kwa mara.
”Kwa sasa mahitaji ya maji katika jiji la Mwanza yani Nyamagana na Ilemela,ni lita milioni 190 kwa siku lakini uzalishaji wetu ni lita milioni 138 kwa siku. Mgao pia unachangiwa na kuyumba na kukatika kwa umeme katika vyanzo vyetu vya maji,”ameeleza Lossindilo.
Amesema kati ya Machi hadi Aprili 20, mwaka huu kumetokea kuyumba kwa umeme mara 26 na kukatika mara 20 katika kituo cha uzalishaji maji Nyakato, ambapo huchukua wastani wa dakika 20-30 kurejesha huduma huku uzalishaji ukisimama kwa wastani wa saa mbili hadi tatu.
”Katika kipindi kama hicho, kwenye kituo chetu cha Butimba kumetokea kuyumba kwa umeme mara 27 na kukatika kwa huduma hiyo mara 17. Tumekuwa na vikao vya kina na TANESCO.Tumejipanga kuondoa mgao kwa kuongeza uzalishaji katika kituo chetu cha Capripointi kutoka lita milioni 90 hadi lita milioni 144 kwa siku,”amesema Lossindilo

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT