Na Joyce Kasiki, Tanga
Nuriath Ahamishaji aeleza safari yake katika WorldSkills
Na Joyce Kasiki, Tanga
MSHIRIKI wa mashindano ya kitaifa ya WorldSkills Nuriath Sheweji kutoka Anna Correction Academy ya Dar es Salaam, amesema ameamua kuingia katika fani ya ubunifu wa mavazi kutokana na mapenzi yake makubwa kwa ubunifu huo, akiamini kipaji hicho ni sehemu ya maisha yake.
Mashindano hayo yameandaliwa na Baraza La Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET) na yameanza Agosti 15 mwaka huu na yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 25 mwaka huu ambapo Mashindano yanatoa fursa kwa vijana wenye ujuzi mbalimbali kushindana, kuonesha vipaji vyao na kujenga uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na kujiajiri.
Nuriath, ambaye ni mbunifu wa mavazi, amesema alianza kujifunza ubunifu huo kupitia mtandao kabla ya kujiunga na chuo hicho kwa lengo la kuongeza ujuzi na kujiandaa zaidi kitaaluma.
Amesema amefika Tanga kushiriki mashindano hayo ya kitaifa yaliyoandaliwa na NACTVET, akiwa miongoni mwa washiriki sita wanaowakilisha fani hiyo, huku akieleza matumaini yake ya kufanya vizuri na kushinda.
“Napenda sana kubuni mavazi na kuwavalisha watu wenye maumbo na ukubwa tofauti. Ubunifu wa mavazi ni kitu ninachokipenda sana,” amesema Nuriath.
Amesema kwa sasa amejikita zaidi katika kubuni na kushona mavazi ya wanawake, wakiwamo akina mama na wasichana, akieleza kuwa bado anaendelea kujifunza na kuboresha uwezo wake.
Nuriath amesema alifikia hatua ya kuingia katika fani hiyo baada ya kusoma hadi kidato cha pili, ambapo aliamua kuelekeza nguvu zaidi kwenye masuala ya mitindo na ubunifu wa mavazi badala ya kuendelea na masomo ya kawaida, uamuzi ulioungwa mkono na familia yake.
Akizungumza kuhusu vijana ambao bado hawajagundua fursa zilizopo katika jamii, amewataka kutumia muda wao kufikiri na kutambua vipaji na mambo wanayoyapenda ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Watumie akili zao, wakae chini wafikiri na watambue kitu wanachokipenda,kuna fursa nyingi ambazo watu hawajui kama zipo, lakini ukikaa na kufikiri unaweza kupata jambo la kufanya,” amesema.
Amesema lengo lake ni kuendelea kujenga ujuzi katika ubunifu wa mavazi na kutumia taaluma hiyo kujenga maisha yake pamoja na kuwasaidia wengine kupitia kazi ya mikono.

More Stories
Mkenda:Ubunifu uzalishwe bidhaa ulete fursa za biashara
TVET yatajwa nguzo ya Uchumi kuelekea Dira 2050
Sound Beat and Soft yazindua duka la vifaa vya muziki Kariakoo