Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Wadau wa uhifadhi na utalii wamepata fursa nyingine ya kuonyesha ubunifu na mafanikio yao baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza rasmi kuanza kwa usajili wa Serengeti Awards 2026.
Usajili utaanza Agosti 20 hadi Septemba 30, 2026, huku wadau wakitakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia tovuti rasmi ya tuzo hizo.
Kwa mwaka huu, jumla ya kategoria 63 katika makundi saba zitashindaniwa, zikiwemo tuzo za waendeshaji wa utalii, waongoza watalii, huduma za ukarimu, uhifadhi, elimu ya utalii na tuzo maalumu za kutambua mchango.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi, amesema tuzo hizo zinafanyika kwa mara ya pili .ambapo mwaka huu ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutambua na kuthamini mchango wa wadau mbalimbali katika uhifadhi wa maliasili na urithi wa Taifa, pamoja na kukuza sekta ya utalii.
Amesema tuzo hizo pia zinalenga kutoa motisha kwa wadau kuendelea kuboresha utendaji wao na kuchangia katika kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoshindana katika soko la utalii duniani.

Akitaja makundi hayo ni Tuzo za Chaguo la Wananchi, Tuzo za Waendeshaji wa Utalii, Tuzo za Waongoza Watalii, Tuzo za Madaktari wa Wanyama, Tuzo za Huduma za Ukarimu, Tuzo za Uhifadhi, Tuzo za Elimu ya Utalii na Tuzo Maalumu za Kutambua Mchango.
Wadau wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na waendeshaji wa shughuli za utalii, waongoza watalii, watoa huduma za malazi na chakula, mashirika ya ndege, taasisi za utalii, vyombo vya habari, waandishi na wahamasishaji wa utalii, kampuni binafsi pamoja na wadau wengine wa uhifadhi na utalii.
Dkt. Mugobi amesema wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaruhusiwa kuwania tuzo hizo iwapo watatimiza vigezo na masharti yaliyowekwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Serengeti Awards, Hatibu Madudu, amesema mwaka huu kategoria zimeongezeka kutoka 56 za mwaka jana hadi 63, baada ya waandaaji kupokea maoni ya wadau na kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali.
Amesema baadhi ya mabadiliko yalitokana na changamoto zilizobainika katika mchakato uliopita, ikiwemo idadi ya wateule au washindani katika baadhi ya kategoria.
Amesema hatua hiyo inaendana na dhana ya utalii endelevu na jumuishi, unaozingatia ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika sekta ya utalii.
“Tunajali utalii endelevu ambao unazingatia makundi yote. Kwa hiyo watu wenye mahitaji maalumu pia wanaruhusiwa kuwania tuzo ikiwa wanajishughulisha na shughuli za uhifadhi au utalii na wanakidhi vigezo vya kategoria wanayowania,” amesema.
Dk. Thereza imewahakikishia wadau kuwa mchakato wa Serengeti Awards 2026 utasimamiwa kwa kuzingatia uwazi, usawa na uadilifu, huku taarifa za washiriki zikihakikiwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko ukizingatiwa..

More Stories
DC Nkasi atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 40
Prof.Mkumbo: Halmashauri zibuni shughuli mpya za kiuchumi si tozo mpya
Maafisa Biashara watakiwa kulinda soko la walaji