Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tabora
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeendesha mafunzo ya siku 3 kwa Watendaji wa uchaguzi kutoka mikoa na hamashauri mbalimbali hapa nchini watakaosimamia uchaguzi wa kujaza nafasi za udiwani na ubunge zilizo wazi.
Akifungua mafunzo hayo yaliyoanza jana katika ukumbi wa Muungano Mess, Mjini Tabora Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania Jacobs Mwambegele, amewataka Watendaji wa uchaguzi huo kutekeleza wajibu wao kwa weledi.

Amewataka kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria ikiwemo kuhakikisha vyama vyote vyenye usajili vinashirikishwa kikamilifu katika uchaguzi huo.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi iliyo wazi ya Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma na Udiwani wa Kata 11 za Tanzania Bara.
Jimbo la Chanwino liko wazi baada ya aliyekuwa Mbunge wao Deogratius Ndejembi kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nawapongeza kwa kuteuliwa ila heshimuni viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, msifanye kazi kwa mazoea, zingatieni Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume,” amesema.
Jaji Mwambegele amewataka kuhakikisha wanatambua mahali uchaguzi utakapofanyikia na kutambua kwa kina vituo vyote vya kupigia kura na kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo hivyo mapema ili viweze kupanga mawakala.
Aidha amewataka kuajiri watendaji wa vituo wenye uwezo na sio kupendelea ndugu, jamaa au marafiki ambao hawana sifa za kufanya kazi hiyo.
Amebainisha washiriki wa mafunzo hayo kuwa ni Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya Jimbo na Kata, Maofisa Uchaguzi, Maofisa Ununuzi na Wahasibu.
Ametaja Kata 11 za Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi wa Udiwani kuwa ni Nonde-Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge-Halmashauri ya Mji Njombe, Bargish-Halmashauri ya Mji Mbulu, Makole-Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mwera-Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.
Nyingine ni Oldonyosambu-Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Igalula-Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shelui-Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mvumi-Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Nyarero- Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu-Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.


More Stories
Watendaji ,viongozi wapewa elimu ya udhibiti
NBS yasisitiza matumizi sahihi ya Takwimu katika Madini
Barrick – Twiga yaunga mkono malengo ya Dira ya Taifa