May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocle Kaijage

NEC yaanza kusikiliza rufaa za wagombea 557

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dsm

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuanza kusikiliza rufaa zilizokatwa na wagombea wa ngazi za ubunge na udiwani kutoka majimboni ambapo hadi sasa tayari imepokea rufaa 557.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocle Kaijage amesema rufaa hizo zimetokana na baadhi ya wagombea ubunge na udiwani kutoridhika na maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi .

“Hadi sasa NEC imepokea rufaa zipatazo 557 ambazo tutaanza kuzifanyia kazi leo (jana) na tutajitahidi kuzitolea uamuzi mapema kwa kadri itakavyowezekana,”amesema.

Wakati huo huo NEC imetoa wito kwa makundi mbalimbali kuendelea kuheshimu sheria za uchaguzi zilizowekwa ili kuhakikisha kila raia mwenye haki ya kupiga kura wanatimiza wajibu wao kikatiba.

“Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , 1977 imeweka masharti ya wajibu wa mtu kufuata na kutii Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano ,” amesema Mhe.Kaijage.

Amesema vivyo hivyo ,Ibara hiyo imeainisha haki ya kila mtu, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria, kuchukua hatua za kisheria kwa madhumuni ya kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi.

Aidha Kaijage amesema kwa msingi huo, malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hizo,yanapaswa kushughulikiwa.

Amesema malalamiko hayo yanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu  kufuata taratibu zilizowekwa .

“Nitumie fursa hii kuwapongeza wagombea wa vyama vya Siasa ambao wamedai haki zao kwa kufuata taratibu za kisheria na za kikanuni katika kuweka pingamizi mbali mbali na hatimaye kukata rufaa NEC,” amesema Jaji Kaijage.

Jaji Kaijage amesema NEC yeye kama kiongozi watashughulikia rufaa zote kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa ujumla Sheria za Uchaguzi na kanuni zake zimeweka masharti, taratibu na hatua za kuchukua panapo kuwa na malalamiko ama ukiukwaji  wa taratibu za Uchaguzi.

“NEC imesema Sheria hizo zimeainisha mamlaka za kushughulikia malalamiko husika, taratibu hizo zimebainishwa katika hatua mbali mbali za uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea hadi kutangaza matokeo,” amesema.

Tume hiyo imesema hivyo wajibu wa wagombea na vyama vyao vya siasa kujua haki zao, mamlaka husika na hatua za kuchukua pale wanapokuwa hawajaridhika na jambo katika kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Katika hatua nyingine Jaji Kaijage alivipongeza vyama hivyo na wagombea ambao tayari wameshaanza kampeni za uchaguzi na wanaendelea nazo, katika maeneo mbalimbali.

Pia amesema NEC inaendelea kuvikumbusha vyama vya siasa na wagombea kufanya kampeni za kistaarabu na zinazozingatia maadili ya uchaguzi.

“Maadili haya wahusika wake wakuu ni Serikali,Tume ya Taifa ya Uchaguzi , vyama vya siasa na wagombea ambapo tume ilikutana mara kwa mara katika vikao mbalimbali na ilivikumbusha kuzingatia makubaliano ya pande zote,”amesema Jaji Kaijage.

“Hivyo NEC imesema wazi kuwa haitarajii kuona vyama vya siasa vikilalamika kuhusu ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi,badala ya kuchukua hatua stahiki za kisheria kwenye mamlaka husika,”amesema.

Tume hiyo imeeleza kuwa hatua hizo ni pamoja na kuzitumia kamati za maadili,ambazo zimepewa mamlaka ya kushugulikia malalamiko yanayohusika ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi hususani katika kipindi cha kampeni.

NEC imebainisha kuwa Kamati za Maadili tayari zimeundwa kuanzia ngazi ya kata kwa uchaguzi wa madiwani,ngazi ya Jimbo-Wabunge na kitaifa kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Makamu wa Rais.

Vile vile imeeleza kuwa kuna Kamati ya Rufaa kwa wagombea ambao hawataridhika na maamuzi ya kamati nyingine.” Kamati hizo zimepewa uwezo wa kuyashughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi kama mlalamikaji  asiporidhika na maamuzi ya kamati katika ngazi husika anaweza kukata rufaa,”amesema Jaji Kaijage.