



Na Jiyce Kaiki,Dar Es Salsam
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Jabiri Bakari, imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja kupitia Dawati Maalum la Huduma kwa Wateja, kwa lengo la kuhakikisha wananchi na wadau wa sekta ya usafiri wa anga wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati.
Akizungumza katika banda la TCAA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja, Bw. Rashid Mngoya, alisema dawati hilo limeanzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka.
Alisema kupitia dawati hilo, wananchi na wadau wanaweza kupata ufafanuzi kuhusu huduma za TCAA, kuwasilisha maoni, hoja na changamoto zao, pamoja na kuelekezwa kuhusu taratibu mbalimbali zinazohusu sekta ya usafiri wa anga.
Mngoya alieleza kuwa Dawati la Huduma kwa Wateja ni sehemu muhimu ya mkakati wa TCAA wa kuimarisha mahusiano na wateja wake kwa kuhakikisha masuala yanayowasilishwa yanapokelewa, kushughulikiwa na kupatiwa majibu kwa wakati.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati. Dawati hili linatoa fursa kwa wananchi na wadau kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka na kupata msaada kuhusu huduma wanazozihitaji,” alisema Mngoya.
Aliongeza kuwa TCAA itaendelea kuisimamia sekta ya usafiri wa anga kwa weledi na ufanisi huku ikizingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama, ulinzi na ubora wa huduma.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TCAA, Bw. Ally Changiwa, alisema Mamlaka imeendelea kuboresha mifumo yake ya mawasiliano na utoaji wa taarifa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wadau.
Alifafanua kuwa miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni kuboreshwa kwa tovuti ya TCAA, ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ikiwa imeongezewa taarifa mbalimbali, hatua inayolenga kuwafikia watumiaji wengi zaidi kwa urahisi.
Aidha, alisema tovuti hiyo imeboreshwa kwa kuongezwa sehemu ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs), inayotoa majibu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kusimamiwa na TCAA.
Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, TCAA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, huduma za kiudhibiti, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege zisizo na rubani (drones), pamoja na masuala mengine yanayohusu sekta ya usafiri wa anga.

More Stories
Mtanzania Avith Philip ang’ara Orodha ya Wajasiriamali 100 Bora Afrika
Zanzibar yatumia Sabasaba kutangaza fursa za uwekezaji
Mwalimu VETA abuni vifaa kusaidia afya na elimu