April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri asimikwa Uchifu, apewa jina la Mshora

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NAIBU Waziri wa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Butiama amesimikwa Uchifu leo na Wazee wa mila wilayani Butiama mkoani Mara na kisha kupewa jina la Chifu Mshora

Wazee hao wameiomba Serikali iwachukulie hatua wanasiasa wanaoleta ukabila, ukanda na udini katika mambo ya maendeleo hali inayoweza kuleta machafuko baina yao.

Wazee hao wameeleza hayo leo wakati wakimsimika uchifu Jumanne Sagini na kumpa jina la Chifu Mshora.

Wakizungumza katika hafla hiyo baadhi ya Wazee wa Mila wamesema kuna wanasiasa wanaotengeneza matabaka baina ya Wazanaki na Wakwaya huku Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipinga vikali vitendo hivyo.

“Sisi kama Wazee wa Mila Wakizanaki tunakemee vikali vitendo hivi vya kibaguzi vya kikabila, kidini na kikanda kwani ubaguzi hauwezi kuleta maendeleo na tunaahidi kuwa bega kwa bega na Mbunge wetu katika kufanikisha Maendeleo ya Wilaya yetu ya Butiama”. Wamesema

Akizungumza baada ya kusimikwa kuwa chifu wa Wazanaki na kupewa jina la Chifu Mshora Mhe. Sagini amesema yupo tayari kushirikiana na Wazee katika jambo lolote hasa ukizingatia kuwa wao ndio waanzilishi wa Taifa hili.

“Wazee wangu nimepokea kwa mikono miwili uongozi huu mliyonikabidhi leo hakika siwezi kuisahau siku hii adhimu katika maisha yangu nitashirikiana nanyi kwa kila jambo katika kuiletea Maendeleo Butiama yetu na niwaonye wale wote wanaodharau Wazee wa Mila kuacha tabia hiyo mara moja kwani hawa ndiyo waliyotulea mpaka tumefika hapa”.

Ameongeza kuwa maji hayawezi kuletwa na udini, miundombinu haiwezi kuletwa na ukabila wala vituo vya afya haviwezi kuletwa na ukanda sisi wote ni ndugu kwa pamoja tuijenge Butiama yetu.