April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

KITUO cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kimeungana na wanawake kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuhimiza wanawake nchini kuwa na utayari wa kujifunza mambo mapya yatakayowawezesha kufikia malengo yao kiuchumi.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kuadhimisha siku hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Kituo hicho Masaki, jijini Dar es salaam juzi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambaye pia Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi SAGCOT, Beng’i Issa mbali ya kuwapongea wanawake wote duniani kwa kuazimisha siku hiyo aliwataka kuwa na utayari wa kujifunza ili waweze kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili kufikia malengo waliyojiwekea.

“Kwanza kabisa ninapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wanawake wote kwa kuazimisha siku hii na ninachukua nafasi hii kuwahimiza kuwa na utayari wa kujifunza ili muweze kukabiliana na changamoto zinazowakabili na kufikia malengo kiuchumi,” amesema Beng’i Issa.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya AKM Glitters, Elizabeth Swai ambayo inajihusisha na ufugaji wa kuku akizungumza juu ya uwajibikaji na kujituma kwa wanawake katika hafla fupi ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani iliyofanyika katika ofisi za SAGCOT makao makuu jijini Dar es salaam.

Amesema kielelezo cha Taifa kuongozwa na Rais shupavu na jasiri kama Mama Samia Suluhu Hassan kinaonesha ni kwa jinsi gani taifa limepiga hatua na kutambua mchango wa wanawake kwenye jamii na kuwataka wanawake wengine kuziangazia changamoto wanazokutana nazo kama fursa ya kupiga hatua kwenye maisha.

“Ni imani yangu kwamba uwepo wa rahisi wetu mahiri kutaleta msukumo chanya kwa wanawake wengine wengi zaidi kutambua kuwa wanaweza na ni suala la kujiamini na kujitambua na kuwa tayari kujifunza”, amesema Beng’i Issa.

Ameongeza kuwa, “Mtaji mkubwa wa mafanikio ni kujituma na kuwa na mahusiano mazuri kazini na adui mkubwa wa kufikia malengo ni uvivu, hivyo ni vitu ninavyotaka niwasihi wanawake wote kuvizingatia ili kuwa na mafanikio”.

Kwa upande Mkurugenzi wa kampuni ya BIG FISH inayojishughulisha na ufugaji wa samaki, Zena Mndeme aliwataka wanawake kutobweteka na shughuli moja bali wajishighulishe na shughuli zingine za uzalishaji ili waweze kuongeza kipato.

“Wengi wetu tunajisahau na kubweteka na kazi pasipo kujishughulisha na ujasiriamali, hii inawanyima waanawake wengi fursa ya kujiongezea kipato, sasa nitoe ushauri kwa wanawake wenzangu kuchangamkia fursa hizi adhimu za kujikwamua kiuchumi”, Amesema Bi. Mndeme.

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGGOT) ambaye pia Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi.Beng’i Issa (katikati) akizungumza katika hafla fupi ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani iliyofanyika katika ofisi za SAGCOT makao makuu jijini Dar es salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha Sagcot, Bi.Anna Mtaita na Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Sagcot Bw.Geoffrey Kirenga

Amesisitiza kuwa “Mwanamke makini ni yule anayejitambua na hasiyetegemezi kwa mwanaume na mwenye kujitambua, kujikubali na kujifunza kufikia malengo kiuchumi”.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya AKM Glitters, Elizabeth Swai amewataka wanawake nchini kuwa na uthubutu kwa kuzichangamkia fursa mbalimbali zilizopo ili waweze kuinua maisha yao kiuchumi.

“Kumekuwa na ofu na wasiwasi mkubwa kwa wanawake wengi pindi wanapotaka kufanya shughuli za ujasiriamali, hivyo basi natoa rai kwa wanawake wote nchini kutokata tamaa na tuwe na uthubutu wa kujaribu kufanya jambo,” Amesema Swai.

Aidha Mkurugennzi Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga amewapongeza wanawake wote kwa kuazimisha siku hiyo na kuwataka kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili waweze kujiongezea kipato.

“Miongoni mwa sekta zilizotoa fursa kubwa kwa wanawake wengi kuweza kushiriki moja kwa moja ni sekta ya kilimo na ufugaji, hii inatoa mwanga kwa wanawake wengine wengi kuona manufaa yaliyopo kwenye sekta hizi ili waweze kunufaika nazo moja kwa moja

SAGCOT ni miongoni mwa taasisi zinazotambua moja kwa moja mchango wa mwanamke kwenye jamii hivyo kwa kuweza kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wanawake pamoja na kutoa mchango mkubwa kwa wanawaek wanao jihusisha na kilimo,mifugo na uvuvi hapa nchini.