April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge waridhia maboresho ya maji Muheza

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Muheza

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava ameridhishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Tanga (Tanga- UWASA) kwa kuboresha upatikanaji wa maji katika Mji wa Muheza.

Amesema jambo hilo linatimiza adhima ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani na kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa karibu zaidi.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akifungua koki ya maji kwenye mradi wa maboresho ya maji Mji wa Muheza.

Ameyasema hayo Aprili 15, 2024 wakati alipotembelea na kukagua mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi katika Mji wa Muheza, ambapo pia aliridhishwa na nyaraka zote za mradi huo ikiwemo kutangaza zabuni kwa njia ya mfumo.

“Mkuu wa Wilaya (ya Muheza Zainab Abdallah), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wote na mara zote ameendelea kuwa na utashi wa hali ya juu sana ya kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi, na kwa sekta ya maji ameendelea kufanya haya mambo kwa vitendo,” amesema Mnzava.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mhandisi wa Tanga- UWASA Violeth Kazumba amesema mamlaka hiyo imetekeleza mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi Mji wa Muheza kupitia ufadhili wa mradi wa kulaza bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanzania (EACOP PROJECT).

Mradi huo una lengo la kuboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi katika Mji wa Muheza ikihusisha kata za Lusanga, Genge, Majengo na Tanganyika zenye wakazi wapatao 21,721 pamoja na eneo la kambi ya wafanyakazi wa bomba la mafuta ghafi.

“Utekelezaji wa mradi huu ulianza Januari, 2023 na kukamilika Septemba, 2023 kwa asilimia 100, ukihusisha uchimbaji wa mtaro mita 6,000, ununuzi na ulazaji wa bomba lenye kipenyo cha 200 mm kwa urefu wa mita 6,000, ununuzi na ufungaji wa viungio vya mabomba, ujenzi wa chemba 15 na ujenzi wa alama za bomba 76 (marker posts) kwa sasa unatoa huduma kwa wananchi,”amesema Mhandisi Kazumba.

Ameeleza kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha milioni 532.55 na umetekelezwa na Mkandarasi Sajo Civil Engineering and Building Construction Company ambaye amelipwa jumla ya 531,357,000″

Wafanyakazi wa Tanga- UWASA, RUWASA na kutoka Wizara ya Maji, wakifurahia maji mara baada ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava kutembelea mradi wa uboreshaji maji Mji wa Muheza

Awali, wakazi hao walikuwa wakipata huduma kupitia bomba la zamani lenye kipenyo cha milimita 160 lililokuwa likipitisha maji ya wastani wa lita milioni 1.5 kwa siku moja katika wiki na sasa huduma ya majisafi inapatikana kupitia bomba jipya lenye kipenyo cha milimita 200 linaloweza kupitisha maji wastani wa lita milioni mbili kwa siku kwa wastani wa siku tatu katika wiki.

Mhandisi wa Tanga- UWASA Violeth Kazumba, akisoma taarifa ya Mradi wa maboresho ya maji Mji wa Muheza