July 3, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akizungumza kwenye kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo na Viwanda na Biashara,Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kagera na Mwanza pamoja na wadau wa kilimo Cha kuzungumza mwenendo wa soko la kahawa nchini, kilichofanyika mkoani Mwanza.Picha na Judith Ferdinand

‘Mwenendo wa soko la kahawa nchini unaridhisha’

Na Judith Ferdinand,Mwanza

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema msimu wa ununuzi na uuzaji wa zao la kahawa ulifunguliwa Juni 9, mwaka huu, ambapo shughuli za ukusanyaji na malipo kwa wakulima zinaendelea kufanyika kupitia Vyama vya Msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo,viwanda na biashara, Makatibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Kagera na wadau mbalimbali wa kilimo kilichofanyika jijini hapa cha kuzungumzia mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa msimu 2020 hadi 2021.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya,akizungumza kwenye kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo na Viwanda na Biashara,Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kagera na Mwanza pamoja na wadau wa kilimo Cha kuzungumza mwenendo wa soko la kahawa nchini, kilichofanyika mkoani Mwanza. Picha na Judith Ferdinand

Kusaya amesema msimu wa ununuzi na uuzaji unatarajiwa kufungwa Machi mwakani,ambapo makusanyo na uzalishaji kwa msimu huu kwa Kanda na mikoa ya Kagera,Songwe ,Mbeya, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha na Kigoma kwa kahawa ghafi wanatarajia kukusanya tani 108,000 ambapo ukusanyaji hadi sasa ni 79,245 sawa na asilimia 73.3 ya lengo waliojiwekea.

Amesema kuwa huku tani za kahawa safi iliokobolewa matarajio yakiwa 70,000 ambapo ukusanyaji hadi sasa ukiwa 44,645 sawa na asilimia 63.85 na zaidi hali ya hewa ilikuwa nzuri na inavyoendelea wanatarajia kuvuka lengo.

“Mifumo mikuu inayotumika na masoko ya kawaha ni miwili ambayo ni wakulima kukusanya kahawa kupitia vyama msingi vilivyopo katika maeneo yao na wakulima kukusanya kupitia vyama vya msingi na kuuza kahawa ghafi kwa wanunuzi binafsi na wenye viwanda ambapo kabla anatakiwa kuwa na kibali lengo la Serikali ni kumtetea mkulima asiweze kupunjika ambapo mifumo inayotumika kwenye kahawa ni miwili ambayo ni mfumo wa soko la moja kwa moja na mfumo wa minada ya kahawa,”amesema Kusaya.

Ameongeza kuwa Wizara kupitia bodi ya kahawa imeboresha na kuruhusu mifumo hiyo miwili ya soko katika ngazi ya awali ili kuongeza ushindani na wakulima hawalazimishwi mfumo wa kuufuata,wameachwa wachague mfumo wanaoona unamanufaa kwao pia Tanzania inauza kahawa nje ya nchi kwa asilimia 93 huku asilimia 7 inauzwa na kutumika ndani ya nchi.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof.Riziki Shemdoe amesema unywaji wa kahawa nchini ni tofauti na uzalishaji kwani asilimia 93 zinaenda nje ,hivyo ajira nyingi zinazalishwa huko japo kuwa zao hilo kutoka nchini linahitajika sana duniani ni wakati wa Watanzania wapende kuitumia kwa wingi kwani unywaji unayofaida sana mwilini.

Alipongeza kuwa msimu huu wamefanya jitihada ambazo hazijawahi tokea kipindi cha nyuma mkulima kupata asilimia 75 , pia wingi wa matumizi utachangia ukuaji wa ajira kwa vijana sambamba na vipato kuongezeka.

Naye Katibu Tawala Mkoa Mwanza Emmanuel Tutuba amesema,Mwanza ni miongoni mwa mikoa 17 nchini inayolima zao la kahawa,ambayo inafaida nyingi na wao kama mkoa baada ya kuona hali ya hewa inaruhusu tayari wameanza kulima zao hilo katika Wilaya mbili na wameona tija inaongezeka.

Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora, amesema inapaswa wananchi kunywa kahawa kwani zinafaida nyingi kiafya na kuongeza thamani ya zao hilo maana wanazalisha lakini asilimia kubwa inapelekea nje ya nchi hivyo inaoaswa angalau robo ya inayozalishwa angalau inyweke na watanzania wenyewe.

“Inapaswa tujielimishe faida kuu za kunywa kahawa,sisi tunazalisha lakini faida wanaenda kupata wengine mfano wenzetu Ethiopia wanazalisha kahawa kuliko sisi na nusu yake wanainywa ndani hivyo tuwe na malengo ya miaka mitatu au minne na sisi kahawa yetu inayozalishwa nchini tuinywe robo, mimi napenda kusema kwamba mikakati endelevu ni kuwa Wizar ya Kilimo,Viwanda na Biashara kuitangaza kahawa yetu ni bora,”amesema.