June 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mv Liemba kufungua fursa mpya za Uchumi Kigoma

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, amesema kukamilika kwa ukarabati wa Meli ya MV Liemba kutaleta mapinduzi makubwa katika huduma za usafiri wa majini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya meli hiyo jijini Kigoma katika maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani, Salum alisema MV Liemba ni tegemeo muhimu kwa maelfu ya wananchi wanaotumia usafiri wa majini kwa shughuli za biashara, usafirishaji wa bidhaa na huduma za kijamii.

Amesema kukamilika kwa meli hiyo kutaimarisha usafiri salama, wa uhakika na wenye ufanisi, huku ikirahisisha mawasiliano kati ya jamii zinazozunguka Ziwa Tanganyika.

“MV Liemba itaendelea kuwa mhimili muhimu wa biashara na maendeleo ya kijamii katika mkoa wa Kigoma na maeneo jirani. Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uchumi wa bluu na kuboresha huduma za usafiri wa majini,” amesema Salum.

Ameongeza kuwa maboresho yanayoendelea kwenye meli hiyo yataongeza uwezo wa kuhudumia wananchi na kuchangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika mkoani Kigoma, yakilenga kutambua mchango wa mabaharia na wadau wa sekta ya usafiri wa majini katika maendeleo ya taifa.