April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga

Muheza wasambaratisha mikusanyiko misiba

Na Steven William, Muheza

MAAFISA wa Idara ya Afya wilayani Muheza mkoani Tanga wamesambaratisha kundi la watu ambao walikuwa wamekusanyika wanajiaanda kula ubwabwa katika msiba wa marehemu Neema George na baadae waende kumzika makaburini.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni katika Kijiji cha Sege wilayani Muheza mkoani Tanga ambako amezikwa marehemu huyo na kundi la wananchi wanaomfahamu kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Marehemu Neema George enzi wa uhai wake alikuwa anaishi katika Kijiji cha Ubena Kata ya Tanganyika wilayani Muheza, lakini kwao kulikuwa katika kijiji cha Sega ambako huko ndio amezikwa baada ya kufa.

Hata hivyo, baada ya Neema George kuumwa na kufariki dunia alipelekwa kuzikwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Sege Kata ya Mbaramo wilayani Muheza na umati wa watu ambao wanamfahamu.

Waombolezaji hao wakati wamejikusanya wanasubiri kula ubwabwa ghafla walitokea Mabwana Afya wawili Omari Mndeme na Shabani Seif wakitumia gari ya Idara ya Afya na kuwasambaratisha wananchi hao bila kula chakula na hivyo kusababisha kwenda kuzika na njaa makaburini.

Afisa Afya huyo Omari Mndeme alisema kuwa, hivi sasa haitakiwi mikusanyiko ya watu katika misiba,kulala matanga wala kupika chakula ambapo watu wanapozika wanatakiwa kuondoka ili kujikinga na maambukizi ya virusi hatari vya ugonjwa wa Corona.

Mndeme alisema kuwa, hivi sasa maafisa wa afya Wilaya ya Muheza wanaendelea na ukaguzi wa kutawanya mikusanyiko ya watu katika misiba,harusi na mambo mengine mbalimbali ili kujikinga na Corona.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanasha Tumbo amepiga marufuku sherehe za harusi na mikusanyiko ya watu kwenye misiba yani kulala Matanga na kupika vyakula ili kudhibiti virusi vya ugonjwa hatari wa Corona katika wilaya hiyo.

Tumbo alisema kuwa, wamekubaliana na viongozi wa dini zote kwamba mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima haifai na kwamba mikutano ya hadhara isimamishwe mara moja kwa muda ya miezi mitatu ili kuangalia hali hiyo ya hatari.

Alisema kuwa, kama kutatokea watu wanataka kufunga ndoa basi watakwenda kufunga kimiyakimiya kanisani ama msikitini na baadae watafanya sherehe baada ya ugonjwa wa Corona kuondoka.

Tumbo alisema kuwa, kunapotokea msiba inatakiwa watu waende wakazike mara moja na hatimae kutawanyika hakuna kuweka matanga na kupika chakula ni marufuku kufanya hivyo ili kuondoa mikusanyiko ya watu na kupeana mikono haitakiwi.

Alisema kuwa, jambo hilo ni kubwa sana linahitaji kutoa elimu ya tahadhari kwa wananchi wa wilaya ya Muheza katika maeneo mbalimbali katika nyumba za ibada na katika mabasi na stendi za mabasi pamoja na shule za msingi,sekondari na vyuo juu ya hatari ya ugonjwa huo.