April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taarifa kwa vyombo vya habari

LATRA:Mabasi zaidi yanahitajika jijini Dar

Na Mwandishi Wetu

ZIKIWA ni siku chache zimepita tangu Serikali kupiga marufuku usimamishaji wa abiria katika daladala hali iliyoleta changamoto kubwa ya usafiri  kwa wananchi Mamlaka ya  Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) imetoa wito  kwa watu binafsi, shule na taasisi  zenye mabasi ambayo hayajapangiwa njia kuomba leseni za muda mfupi ili kutoa huduma za usafiri.

Marufuku hiyo ni hatua ilkiyochukua Serikali katika kukabiliana na  kuenea kwa virusi vya Corona (Covid-19) ambapo tayari  imesababisha  kifo cha mtu mmoja huku watu 19 wakiambukizwa virusi nchini.

Hayo yalibainishwa jana kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,Gilliad Ngewe  ikiwataka watu wenye mabasi ya abiria ambao hawajapangiwa njia kufika ofisi za LATRA kuomba leseni kusudi kuanza kutoa huduma hiyo.

Hivi karibuni LATRA iliagiza mabasi yote yaendayo haraka kupitia Mradi wa BRT na daladala zote kubeba abiria kulingana na idadi ya viti vilivyopo ukiwa ni mkakati wa kukabiliana na kusambaa kwa COVID-19.

Pia iliagiza  kila chombo cha usafiri kiwe na dawa ya kutakasa mikono ili kabla ya abiria kuingia ndani ya basi aweze kutakasa mikono.

Ngewe alisema, utekelezaji wa agizo hilo ni hatua ya kujikinga dhidi ya virusi vya Corona katika vyombo vya usafiri.

“LATRA imekutana na wadau wa usafiri na usafirishaji ardhini na kutafakari kuweka mikakati ya kukabiliana na janga hili, wamiliki wote na wafanyakazi wao wanaagizwa kuhakikisha wananyunyizia mabasi yao dawa kila mwisho wa safari.

“Pia Shirika la Reli Tanzania -(TRC) na Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) wahakikishe treni  zinapulizwa dawa kila mwisho wa safari,”alisema.

Mbali na hilo kwa magari ya mizigo, Ngewe  alisema hayaruhusiwi kubeba abiria yeyote huku akisistiza elimu juu ya kujikinga na virusi vya  Corona itolewe ndani ya vyombo vya usafiri kwa kutumia rradio na runinga katika magari hayo.

“Lakini  hatua nyingine haitoruhusiwa kuanzia sasa watu wanaomsindikiza abiria kuingia katika vituo vya treni au mabasi yaendeyo mikoani,”aliongeza.