April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Maji Mababu Kyera wamridhisha kiongozi mbio za Mwenge

Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Kyela

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021, Luteni Josephine Mwambashi ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji Mababu wilayani Kyela mkoani Mbeya na kuagiza mwishoni mwa mwezi huu mradi huo ukamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. 

Luteni Mwambashi ameyasema hayo jana mara baada ya Mwenge wa uhuru kutembelea mradi huo kwa lengo la kukagua utekelezaji wake.

“Mradi huu ulipitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2019. Leo tulikuja kuangalia hatua iliyofikiwa na kujiridhisha iwapo unatekelezwa katika viwango vilivyokusudiwa, tumeridhishwa na utekelezaji hivyo hadi mwishoni mwa mwezi huu mradi huu uwe umakamilika na wananchi wapate huduma ya maji,” amesema Luteni Mwambashi.

Aidha, kiongozi huyo amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya maji ili isiharibiwe.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye pia ni mbunge kupitia viti maalumu wanawake mkoa wa Mbeya amemhakikishia kiongozi  huyo kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.

Amesema mradi huo ulikuwa na vituo vitano vya kuchotea maji, Serikali chini ya Rais Samia iliongeza fedha kiasi cha sh. milioni 207 ambazo zimewezesha kuongeza miundombinu ya mabomba, tenki la kuhifadhia maji pamoja na vituo vinne zaidi vya kuchotea Maji kutoka vitano vilivyokuwa katika bajeti ya awali. 

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Luteni Josephine Mwambashi akizindua mradi wa maji wa wa Mababu wilayani Kyera, mkoani Mbeya.

Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini Wilaya ya Kyera Mhandisi, Tanu Deule amesema mradi huo unatarajia kuhudumia wakazi 5,121 kutoka vitongozi vitano vya kijiji cha Mababu ambapo gharama ya utekelezaji inatarajiwa kuwa zaidi ya shilingi  milioni 398.

Mwenge Maalumu wa Uhauru uko mkoani Mbeya ukitarajia kukamilisha mbio zake kesho.