September 26, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RAAWU waomba kuendelea kushirikiana na Serikali

Na Esther Macha, Timesmajira,Online ,Mbeya

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Ushauri (RAAWU), Winston Makere  ameiomba Serikali  kuendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi katika kutatua changamoto zinazojitokeza mara kwa mara mahali pa kazi .

Makere amesema hayo jana wakati akisoma risala ya ufunguzi kwa mgeni rasmi wakati wa semina ya siku tano kwa viongozi na wawakilishi wa matawi ya  vyama vya wafanyakazi ambayo inafanyika mkoani Mbeya katika ukumbi wa chuo cha Uhasibu Mbeya .

Katibu huyo Makere amesema chama hicho kina wanachama 10,000 nchi nzima na kiutendaji kimegawanyika katika ngazi tatu, ambazo ni Tawi, kanda  na Taifa.

Amesema kijiografia wana kanda tano ambazo ni Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Zanzibar, Kanda ya Kaskazini ni Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara na kwamba kanda ya kati ina Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida,Tabora, na Kigoma

Aidha Makere ametaja Kanda ya Ziwa kuwa ina mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera,Shinyanga, Geita na Simiyu, kanda nyingine ni Nyanda za Juu Kusini  ambayo mikoa yake ni Mbeya, Ruvuma ,Iringa, Rukwa,Songwe, Njombe na Katavi.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Ushauri (RAAWU), Winston Makere  (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutanuo huo, Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson.

“Ndugu mgeni rasmi tunaamini taasisi yako ni mhimili unaojitegemea, hivyo tunaomba iendelee kutunga sheria ambazo ni rafiki kwa wafanyakazi na Taifa kwa ujumla,“amesema  Makere.

Akizungumzia kuhusu changamoto Katibu Mkuu huyo amesema baadhi ya waajiri kutopenda uwepo wa chama mahali pa kazi hali inayopelekea uvunjifu wa haki za wafanyakazi, kutokuwepo kwa chombo kimoja kinachodhushulikia migogoro ya wafanyakazi mfano watumishi wa umma mchakato wao ni tofauti na watumishi wa sekta binafsi.

Akifungua semina hiyo siku tano kwa wawakilishi wa matawi ya  vyama vya wafanyakazi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya, Dkt. Tulia Ackson amesema viongozi lazima wajue namna ya kutunza fedha wanazopokea kwa waajiri, kwani siku zote fedha huwa hazitoshi .

Aidha Dkt. Tulia amesema kuna changamoto kwa waajiri kuendelea kupata elimu hiyo itasaidia wafanyakazi wakiwa na sehemu ya  kusemea matatizo yao.

Hata hivyo Naibu spika huyo amepongeza wanawake ambao ni viongozi wa matawi ya wafanyakazi na kuwataka kufanya kazi kwa uaminifu na nidhamu na bidii na wale walio nyuma yao kuwaamini waone kuwa wamefanya njia sahihi ya kuwachagua wanawake.