April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Livinglab wakabidhi ramani za kidijitali kata tisa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Tanga

KATA tisa za Mkoa wa Tanga zimepokea ramani za kidigitali zinazoonesha taarifa za maeneo na mifumo taarifa za kijografia (GIS) ili kusaidia katika kuboresha huduma za ukusanyaji taka ngumu na utambuzi wa maeneo hatarishi kiafya na kiusalama.

Ramani hizo pia zinaonyesha taarifa za maeneo muhimu, mitaa na majengo pamoja na mifumo ya kusimamia mipango ya maendeleo ya Jiji la Tanga.

Kata hizo ni pamoja na kata ya Chumbageni, Central, Ngamiani Kaskazini, Ngamiani Kusini na Ngamiani Kati. Zingine ni Majengo, Usagara, Duga na Nguvumali.

Mkurugenzi wa Tanzania Data Lab, Stephen Chacha, amesema kuwa mradi huo wa LivingLab Initiative una lengo la kuwezesha matumizi ya data kufanya maamuzi mkoani Tanga.

Amesema mradi huo wa Livinglab unatatajiwa kulifanya Jiji hilo kuwa la kimataifa kwa usafi na kwa mpangilio wake na madi huo wa miaka mitatu unatekelezwa kwa pamoja na Halmashauri ya Jiji la Tanga, Chuo Kikuu Ardhi na Tanzania Data Lab kwa ufadhili wa Fondation Botnar ya Uswis.

Amesema mbali na kulipaisha Jiji hilo kimataifa, pia unatarajiwa kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana wa mkoa huo ambao wamekuwa wakishirikishwa kila hatua ya mradi huo.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliowashirikisha madiwani na watendaji wa wa Jiji hilo, Chacha amesema vijana waliotumika kukusanya taarifa na takwimu hizo ni kutoka Chuo Kikuu Ardhi (ARU) na vijana wa Mkoa wa Tanga.

Amesema vijana hao wamefanyakazi kubwa kwa ufanisi wa hali ya juu kuibua fursa mbalimbali za Mkoa wa Tanga na kutoa takwimu na taarifa ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwenye mipango miji.

Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Joseph Colyvas (kulia) akiwa ameshika ramani ya kidigitali yenye taarifa za kijografia kwenye kata zao akiwa na madiwani wenzake wa Tanga waliyokabidhiwa kwenye mradi wa Livinglab unaoendeshwa na Tanzania Data Lab, Chuo Kikuu Ardhi (ARU) na Jiji la Tanga unaofadhiliwa na Foundation Botnar ya Uswisi. Na mpiga picha wetu.

Amesema kabla ya kuanza kwa mradi huo Jiji la Tanga lilikuwa katika hali mbaya kimpangilio lakini baada ya mradi huo mtu anaweza kutafuta mtaa na taarifa mbalimbali za Mkoa huo kiganjani mwake.

” Sasa hivi unaweza ukaingia kwenye simu yako ukatafuta taarifa mbalimbali za Mkoa wa Tanga, mitaa imeanishwa na kila nyumba na inatumika kwa biashara gani viko mtandaoni,” amesema.

Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Joseph Colyvas alisema mradi huo ni muhimu kwani umeliweka Jiji la Tanga kwenye ramani ya dunia.

Amesema mradi huo umeibua mambo mengi zikiweno sehemu ambazo si salama, maeneo ya wazi, na maeneo ya utupaji taka. Hali hii itasaidia sana hata kupunguza migogoro ya ardhi.

“Botnar wametuambia leo kwamba kuna bilioni 7 zinatarajiwa kuletwa kwaajili ya maendeleo ya Tanga. Tunawashukuru sana kwani hadhi ya Jiji letu itapaa na pengine kuyapita majiji mengine,” amesema Naibu Meya.

“Tumemwelekeza mtu wetu wa IT kwamba hizi takwimu na taarifa aziweke kwenye kanzidata yetu maana zitatusaidia sana kupata hata wawekezaji,” amesema

Aidha, Naibu Meya huyo amewaomba madiwani na watendaji wa Jiji la Tanga kuhakikisha wanashirikiana kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Botnar ili wasioneoke nchini. Aliwaomba wawakilishi wa Fondation Botnar kuandaa mafunzo zaidi hata kwa madiwani ambayo kata zao hazijapitiwa na mradi huo ili waweze wawe na uelewa wa pamoja kuhusu mradi huo.