May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aisha Musa al-Saeed. (Picha na EBRAHIM HAMID/AFP/GETTY IMAGES).

Mpasuko waendelea Serikali ya Sudan

KHARTOUM, Mwanachama raia wa Baraza Kuu la Utawala la Sudan, Aisha Musa Sayeed amejiuzulu akidai amelazimika kufanya hivyo kutokana na kuingiliwa kati kwa kazi yake na maafisa wa jeshi katika serikali ya mpito.

Sayeed amewatuhumu viongozi wa kijeshi kwa kuwaweka kando raia na kufanya maamuzi ya upande mmoja yanayoathiri nchi nzima ikijumuisha matumizi ya nguvu ya hivi karibuni dhidi ya waandamanaji wa amani.

Mwanachama huyo amewaeleza waandishi wa habari mjini Khartoum kuwa,aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa sababu upande wa jeshi katika baraza la utawala ulipuuza maoni ya wanachama wengine wa baraza.

Sayeed ni raia wa tatu mwenye cheo cha juu nchini Sudan kuondoka kwenye wadhifa wake katika muda wa wiki moja.

Awali Mwanasheria Mkuu wa Sudan, Taj Al Sir Al Hibir alijiuzulu akieleza kuingiliwa katika kazi zake kutoka idara zisizoidhinishwa na serikali, katika ofisi ya mwendesha mashtaka ya umma, ambapo aliita ni ukiukaji wa wazi wa sheria na Jaji Mkuu, Neimat Abdallah Mohammed Khair aliondolewa na baraza kuu.