May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Momba waja na mkakati mpya kuongeza mapato

Na Moses Ng’wat, Momba.

BARAZA la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Momba kwa kauli moja limepitisha mfumo mpya wa ukusanyaji mapato utakaoshirikisha ngazi za vijiji na kata, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Uamuzi huo ulifikiwa Mei 7, 2026 wakati wa kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26 kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya mfumo huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Fabiani Manoza, Ofisa Mapato, Frank Wakusongwa, alisema utekelezaji wa mfumo huo utaimarisha usimamizi wa mapato kwa kuwashirikisha moja kwa moja watendaji wa kata na vijiji.

Alifafanua kuwa ajira za wakusanya mapato zitafanyika katika ngazi ya kata, ambapo watendaji wa kata watakuwa na jukumu la kutangaza nafasi, kuajiri na kusimamia wakusanya mapato kwa kushirikiana na Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC).

Kwa mujibu wa Wakusongwa, wakusanya mapato hao watasaini mikataba ya muda wa miezi mitatu kulingana na utendaji kazi wao, huku malipo yao yakitokana na asilimia 10 ya mapato yatakayokusanywa na kurejeshwa katika kata husika.

Aliongeza kuwa halmashauri itarejesha asilimia 10 ya mapato yote yatakayokusanywa na kupelekwa benki, fedha zitakazotumika kugharamia shughuli za ukusanyaji, kulipa watendaji na kutekeleza miradi ya maendeleo katika kata na vijiji.

Wakusongwa, amesema ili kudhibiti upotevu wa mapato, halmashauri imeweka adhabu kali kwa watakaobainika kukwepa au kutorosha mapato, ikiwemo faini kwa wanunuzi wa mazao, wakusanya mapato na wamiliki wa vyombo vya usafiri.

Hata hivyo, baraza limeidhinisha jumla ya Sh milioni 42 kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mfumo huo, ambapo kila kata kati ya 14 itapatiwa Sh milioni 3. Utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika ndani ya robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2025/26 na robo ya kwanza ya 2026/27.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Halmashauri, Sabina Mwajeka, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uadilifu katika mchakato wa kuwapata wakusanya mapato ili kupata watu waaminifu watakaosaidia kuongeza mapato ya halmashauri.

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri, Sylivester Haizuru, aliwataka madiwani kusimamia kwa karibu mchakato wa upatikanaji wa wakusanya mapato katika maeneo yao, huku akionya dhidi ya vitendo vya upendeleo na kuingiza watu kwa maslahi binafsi.