
Na Moses Ng’wat, Ileje.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoani humo, pamoja na Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Isongole–Isoko yenye urefu wa kilometa 52 kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 73.
Makame ameeleza kutoridhishwa na maendeleo ya mradi huo baada ya taarifa kuonesha kuwa upo nyuma kwa zaidi ya asilimia 48 ya utekelezaji uliopangwa.
Akizungumza Mei 7, 2026, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku mbili wilayani humo, Makame alisema kasi iliyopo hairidhishi licha ya mkandarasi huyo tayari kalipwa sehemu ya fedha za mradi kiasi cha Sh bilioni 7.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeonesha dhamira ya dhati kwa kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo, ambao ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Ileje.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza Tanroads Mkoani humo kuimarisha usimamizi wa mradi huo, huku akimtaka mkandarasi kuhakikisha vifaa vyote muhimu vinawasilishwa eneo la mradi kwa wakati ili kuongeza kasi ya utekelezaji.
Aidha, alihoji sababu za kutokuwepo kwa Meneja wa Mradi kwa zaidi ya wiki mbili, akieleza kuwa hali hiyo inadhoofisha usimamizi wa kitaalamu wa utekelezaji wa mradi huo muhimu.

“Serikali imeshatoa fedha, sasa tunataka kuona kasi ya utekelezaji inaendana na thamani ya mradi huu,” alisisitiza Makame.
Alielekeza kuwepo kwa usimamizi wa karibu ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje.

More Stories
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77
Wafugaji watakiwa kulinda ardhi yao