April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkoa wa Pwani na mkakati wa kukuza zao la muhogo

KATIKA kuhakikisha inatumia na kufaidika na soko la kimataifa la muhogo linalotumika kuunganisha chuma, Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wakulima,kujenga viwanda vya kusindika zao hilo ili kuongeza usafirishaji wa bidhaa.

Serikali inasema kuwa mahitaji ya zao la muhogo na bidhaa zake katika soko la kimataifa ni kubwa kwa sababu matumizi yake katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji.

Muhogo hautumiki tu kwa chakula bali unatumika katika shughuli za kuunganisha chuma na mbao ambapo mahitaji makubwa yako Ulaya, Marekani na China.

Kwa sasa zao la muhogo limepewa kipaumbele maalum duniani, kutokana na muhogo hausindikwi kutengeneza unga wa ugali, uji, mkate na biskuti pekee yake. Unga wa muhogo siku hizi unatumika kwenye uunganishaji wa chuma, mbao, kutengeneza gundi na matumizi mengine mengi sana.

Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa ya Tanzania bara inayoongozwa kwa uzalishaji mkubwa wa zao la Muhogo. Mikoa mingine ni Tanga, Lindi, Mtwara, Morogoro na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa sasa inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuongeza tija na uzalishaji ikiwemo kuongeza uzalishaji kutoka tani sita kwa hekta moja hadi kufikia tani kumi na tano mpaka ishirini.

Aidha, serikali inashauri wakulima wote wa zao la muhogo na mazao mengine kuzalisha mazao yao kwa kuangalia mahitaji ya soko ikiwa ni pamoja na kuzalisha mazao ya kutosha, udhibiti wa visumbufu vya wadudu, magonjwa pamoja na usafi wa mazao hayo.

Pia serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikiainisha masoko ya ndani na nje ili mkulima aweze kuboresha kilimo chake na kulifanya soko liwe la uhakika.

Hivi karibuni soko la muhogo limeongezeka kwa mfano Tanzania imepata fursa ya kuuza muhogo nchini China, masoko hayo yanahitaji kiwango kikubwa cha muhogo lakini wenye sifa stahiki.

Ni kwa muktadha huo Mkoa wa Pwani umeanza uhamasishaji wa uwekezaji katika zao la muhogo ili kuwawezesha wakulima kujiongezea kipato na wakati huo kuendanana soko la China.

Kutokana na changamoto hiyo tayari Serikali imefanikiwa kupata soko la uhakika katika kiwanda cha kuchakata mhogo kilichopo Mkenge kata ya Veta wilayani hapo ambapo uzalishaji wa muhogo mkoani humo ni tani 900,000 hadi milioni 1.2 .

Akihimiza kilimo hicho Mkuu wa Mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ambaye alikuwa kwenye ziara ya kuweka mawe ya msingi katika baadhi ya viwanda anasema soko la muhogo lilikuwa duni na wakulima walikuwa wakilima kwa wingi bila kupata faida.

“Kiwanda hiki kitatoa ajira,pia bei ya mhogo itakuwa yenye tija kwa kuwa watatumia kupima kwa mzani, kwa sasa bei haitabiliki ikiwa lumbesa 60,000 hadi 80,000 ,suzuki 300,000 ambapo kwa hali hiyo ni bei inayomlalia na kumnyonya mkulima huyu wa Mkuranga”anafafanua Ndikilo.

Hata hivyo anaeleza ,moja ya malengo ya ziara yake ni kudhihirisha Pwani inakwenda kuwa ukanda wa viwanda pamoja na kuithibitishia dunia kwamba Tanzania ni eneo linalovutia kwa viwanda.

Awali mhasibu wa kiwanda cha Tanzania Huafeng agriculture development Ltd,Leonard Jabee ,alieleza kiwanda kinamilikiwa na wachina ,kilianza ujenzi march 2019 na utakamilika mwishoni mwa mwaka huu,utagharimu bilioni 9.1.

Alielezea, wataanza kutengeneza vipande vya mhogo na kisafirisha China kisha kuzalisha wanga na kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 200 kwa siku kupitia Amcos za wakulima huku wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme.

China pekee inahitaji tani 2.5 za muhogo kwa mwaka ambapo amesema wanaongeza kasi ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao la muhogo ili kuongeza thamani ya zao hilo na biashara ya kimataifa.

Katika kuhakikisha wanafikia hazma hiyo, Serikali inaendelea kuwawezesha wakulima kwa mitaji na kutoa elimu ya kilimo bora cha muhogo, utafiti, kutumia mbegu bora ambapo Wizara ya Viwanda na Biashara na Kilimo zinashirikiana kuhakikisha mkulima anaongeza uzalishaji kutokana na elimu inayoipata.

Serikali imeweka vipaumbele vitatu ambavyo vimewekewa msisitizo wa uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Vipaumbele hivyo ni; viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani sambamba na kulinda jasho la mkulima.

Kipaumbele cha pili ni kutengeneza bidhaa za majumbani kama vyakula, nguo, mafuta ya kula, viatu, samaki na vifaa tegemezi katika sekta ya ujenzi kama thamani za viti, mabati ili kuharakisha ubora wa maisha na maendeleo. Na kibaumbele cha tatu ni viwanda vinavyoajiri watu wengi ili kuhakikisha ajira kwa vijana.

Kwa hapa Tanzania, muhogo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuna, Tanga, Morogoro, Shinyanga ambapo hutumika kama zao la biashara na wakati huohuo ni zao la chakula.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Uzalishaji wa Chakula kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 iliyotolewa na Wizara ya Kilimo Februari 2019 inaeleza kuwa katika msimu wa kilimo wa 2017/2018 uzalishaji wa zao la muhogo ulikuwa tani 2.7 milioni ambapo Mkoa wa Kigoma uliokongoza kwa kuzalisha tani 445,526 sawa na asilima 15.9 ya uzalishaji wote katika kipindi hicho.