May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga akizungumza na mwandishi wa makala haya ofisini kwake kuhusiana na mkakati wa Wilaya hiyo katika kuzuia vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto.

Hivi ndivyo mwanafunzi alivyotumbukia kwenye biashara ya kuuza mwili alivyookolewa na Afisa Tarafa

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online

UKATILI dhidi ya watoto umeenea sana ulimwenguni na kusababisha ongezeko la vifo vya watoto vinavyotokana na ubakaji ama kushiriki kwenye ngono wakiwa na umri mdogo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema kuwa watoto ndio wanaoathirika sana duniani kutokana na sababu mbalimbali.

Ofisa Tarafa wa Ngudu Wilayani Kwimba Hamza Hussein akizungumza kuhusiana na vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto. Picha zote na Judith Ferdinand

TimesMajira hili iligonga hodi katika Kijiji cha Bugakama Kata na Tarafa ya Ngudu Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza na kukutana na binti mwenye umri wa miaka 13 na mwanafunzi wa darasa la saba katika shule moja ya msingi wilayani hapo aliyeitwa Mkatesi Shukuru(siyo jina lake halisi) ambaye anaelezea namna makundi rika,picha za ngono pamoja na hali duni ya maisha ya mama yake na kujiingiza katika biashara ya kuuza mwili ili kupata fedha.

Akizungumza na TimesMajira Shukuru, anasema kuwa alianza kujiingiza kwenye tabia hiyo akiwa darasa la sita mara baada ya marafiki zake kumshawishi na kumtaka afanye kama wao wanavyofanya ili aweze kupata fedha ya kununulia chakula kizuri pamoja na taulo za kike.

Anasema kuwa baada ya kuvunja ungo alimuomba mama yake fedha kwa ajili ya kununulia taulo za kike lakini kutokana na hali duni ya maisha mama yake ambaye ndiye mzazi pekee aliyebaki baada ya baba yake kufariki akiwa na umri mdogo alishindwa kutekeleza ombi hilo.

Anasema kuwa kutokana na kukosa aliona njia bora ni kutumia mwili wake kukidhi mahitaji yake muhimu ambapo alikua analipwa sh.2000 hadi 4000 kila anaposhiriki tendo la ndoa.

Pia anasema sababu nyingine iliyomsababishia kujiingiza huko ni kutokana na marafiki zake waliokuwa kidato cha nne na wengine darasa la saba kumuonesha picha za ngono kupitia simu zao na huku wakiwasifia wapenzi wao.

“Wenzangu walikuwa wapenzi wao nami niliingiwa na tamaa na kuvutiwa na simulizi hizo hivyo kujikuta kwenye vitendo hivyo na matokea yake nikajikuta nikuza mwili kwa wanaume tofauti tofauti.

“Fedha nilizokuwa napata nilikua nanunulia wali nyama na taulo za kike, mimi ni mtoto wa mwisho kuzaliwa kati ya watano ambapo baba yangu alifariki wakati nikiwa mdogo na mama yangu ni mkulima ambaye ana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

“Nilianza tabia hiyo mwaka jana baada ya kukosa fedha ya kununua taulo ya kike na kupokea ushauri kutoka kwa baadhi ya marafiki zangu ambao walikuwa wakielezana namna ya kushiriki kwenye tendo la ndoa na wanavyopata fedha kutoka kwa wanaume.

“Kuna wakati mwingine nililazimika kumsingizia mama yangu kuwa ni kipofu ili iwe rahisi kwa watu ninaokutana nao waweze kunipatia fedha kwa haraka na urahisi pamoja na kunionea uhuruma ingawa baadhi yao walinitaka kingona ambapo nilikuwa nawakubalia kisha wao wananipatia kiasi cha fedha kuanzia sh.2000 hadi 4000.

“Darasani nilikua nafanya vizuri tu nashika nafasi ya 13 kati ya wanafunzi zaidi ya 100, nilijihusisha kimahusiano na watu wazima lakini sasa najuta…….nahitaji kuwa mtoto mwema,nisome na nitimize ndoto yangu ya kuwa mwalimu na niweze kuisaidia familia yangu na mama yangu” anasema.

Hata hivyo anawaasa watoto wenzie wa kike kutojiingiza katika vitendo kama hivyo na badala yake waridhike na hali ya maisha ya nyumbani kwao na kujikita katika kusoma na wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kuzungumza nao na siyo kuwa wakali tu huku Serikali na wadau wengine wahakikishe elimu ya makuzi,afya ya uzazi na kukitambua ianze kufundisha kuanzia ngazi ya familia,shule ya msingi na kuendelea.

Kwa upande wake mama mzazi wa Mkatesi Shukuru akizungumza na Majira lilipomtembelea nyumbani kwake mama mzazi wa binti huyo Neema Abel (Siyo jina lake halisi) anasema kutokana na tabia alioinza binti yake mwaka jana kama mzazi ilibidi atumie ukali kama vile kumpiga,kumfungia nje pia kumshirikisha rafiki yake ambaye alimuonya na kumuelimisha lakini alibadilika kwa muda mfupi na baadae alianza tena.

“Nimelea watoto vizuri tu kama dada zake na kaka zake lakini huyu …..mmmmh! na mabadiliko yake yalikuwa ya ghafla mmo na tabia yake hiyo kama mzazi inaniumiza sana.

“Mwanangu mwanzo hakuwa na tabia mbaya alikuwa anajiheshimu anapenda kusoma Bibilia muda wote lakini alikuja kubadilika ghafla mtaani wananisema sana lakini imani yangu atabadilika na kuwa mtoto mwema darasani alikuwa anafanya vizuri sana na muda anaotoka kufanya mambo yake ni anategea nikitoka na yeye anatoka na anarudi kabla sijarudi na wakati mwingine anasingizia kuwa alikua ameenda kujisomea kwa wenzie,” anasema.

Anasema, amekuwa akimpa elimu juu ya afya ya uzazi na kukitambua ila anahisi pengine uwasilishaji wake siyo mzuri labda ndio sababu ya mtoto huyo kujiingiza katika masuala hayo pia aliwai kuombwa na mtoto wake huyo pesa za kununukia taulo za kike anakuwa hana kutokana na hali duni aliyonayo kwani awali alikuwa akifanyakazi lakini alipunguzwa na kuamua kujikita kwenye kilimo tu.

Naye Ofisa Tarafa ya Ngudu Wilayani Kwimba Hamza Hussein anasema changamoto kubwa zilizopo kwenye tarafa hiyo ni watoto kujihisisha katika masuala ya mahusiano na kujikuta wakiangukia kwenye vitendo vya ukatili wa kingono hasa kwa wanafunzi hiyo inatokana na wazazi kutowajibika ipasavyo katika malezi kwani wengi wao wanawapa sana uhuru watoto wao.

Hamza anasema chanzo kingine ni utandawazi,tamaa ya watoto hao inayochangiwa na kukosa fedha za kununulia mahitaji muhimu ya watoto hao wa kike ikiwemo nguo za ndani na taulo za kike na vyakula vizuri tofauti na vile vinavyopatikana nyumbani.

“Huyo binti alikuwa ananikimbia kila ninapokutana naye kwa sababu ninawakamata na nimempa elimu na ameahidi kubadilika na natumaini atabadilika mwanzo alinidanganya kuwa mama yake ni kipofu hali iliyopelekea yeye kujiingiza katika biashara hiyo katika umri mdogo ili kuweza kuhudumia familia.

“Lakini sikuchoka kumfuatilia na nikabaini ukweli hivyo niliongea naye akanieleza kila kitu na sitochoka kumfatilia na kuwafatilia watoto wengine kwani tunahitaji kuwa na watoto wakike wasomi na wenye kushika nafasi mbalimbali katika uongozi,”anasema Hamza.

Anasema mikakati yao ni kutoa elimu kwa jamii sanjari na kufanya msako kwa wale wanaowashawishi watoto hususani wa kike kufanya kushiriki tendo la ndoa kwenye umri mdogo na kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Ofisa Tathimini na Ufuatiliaji wa Mradi wa Boresha unaotekelezeka na Shirika la Tanzania Interfaith Partnership (TIP) Wilaya ya Kwimba Respectson Akyoo anasema mradi huo ulianza mwaka jana Oktoba na kwa wilaya hiyo unatekelezwa kwenye kata 18 kati ya 30 zilizopo na wanafanya kazi kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii,Polisi,Dawati la Jinsia wilaya,wahudumu wa afya na wasaidizi wa kisheria ambao unavipaumbele viwili ikiwemo ulinzi na usalama na watoto huku katika hilo wakijikita katika ukatili wa kingono kwa watoto ambao hupelekea kushamiri kwa maambukizi ya virusi vya VVU.

Anasema tangu kuanza kwa mradi huo wameisha ripoti zaidi ya kesi 100 zinazohusu na vitendo vya ukatili hususani wa kingono kwa watoto huku wakibaini sababu zinazopelekea vitendo hivyo ni pamoja na umaskini, taarifa kutotolewa,hofu ya kutoa taarifa,imani za kishirikina na baadhi ya wazazi kuwatumia watoto wao kama chanzo cha kuwaingizia kipato hivyo kuchochea mtoto kujiingiza kwenye mahusiano mwisho wa siku kufanyiwa vitendo vya kikatili wa kingono.

Pia anasema,wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii kwa ili kuwajengea uelewa kuhusiana na masuala ya ukatili hasa wa kingono huku wakifanikiwa kutoa i kupitia taasisi za kidini, vikundi vya kukopa na semina na idara ya afya,Polisi na Ustawi wa Jamii ili kuleta hamasa na uelewa kwa jamii.

Aidha Ofisa Mradi wa Boresha Wilaya ya Kwimba Hamisi Kibayasi anasema wakati umefika wa jamii kupewa elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya ukatili dhidi ya watoto kwani wapo wanapofanyiwa pasipo wao kujua huo ni ukatili pia elimu ya ukatili ikianza kutolewa kuanzia ngazi shuleni itasaidia kuondokana na adha hizo.

“Sisi tumekutana na kesi nyingi zinazowahusu watoto kufanyiwa ukatili lakini shirika letu limeanza kutoa elimu kwa watoto ambao wapo kwenye elimu ya dini Jumapili na Madrasa tunawaelimisha walimu nao wanatoa kwa wanafunzi lengo elimu hiyo iweze kufika chini na itawasaidia watoto kujitambua na kujua ukatili ni nini ,tunapendekeza elimu hii ianze kutolewa shuleni itawasaidia watoto kutambua ukatili ni nini,kujikinga , kujiepusha na kuondokana na ukatili ” anasemaa Kibayasi.

Mchungaji wa kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania (P.A.G.T) Ngudu wilayani Kwimba Elias Shileka anasema suala la watoto wenye umri wa kuanzia miaka 12 hasa wa kike kujiingiza katika mahusiano limekuwa tatizo kubwa lenye kuleta mmomonyoko wa kimaadili katika jamii mara nyingi suala hilo linapelekea kukatishwa kwa masomo yao kwa kudanganywa na vitu vidogo .

“Unakuta mzazi anampa uhuru uliopitiliza mtoto lakini wakati tulionao ni wa kuomba na kuwatanguliza watoto katika maombi yao ili tuwe na kizazi kilichochema na kimpendezacho Mungu”anasema Shileka .

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga anasema ili kuondokana na changamoto ya ukatili wa kingono kwa watoto hususani kike wanajikita katika kuzuia zaidi kwa kutoa elimu kwa watoto wa kike na jamii kwa ujumla pamoja na kujenga mabweni kwenye shule za sekondari kwa ajili ya watoto wa kike kuwapunguzia umbali wa kutembea ambao ni moja ya sababu inayochangia binti kujiingiza kwenye vitendo hivyo kutokana na ushawishi anaoweza kukutana nao njiani.