May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milango zaidi kufunguka hifadhi ya Taifa Ruaha kupitia REGROWN

Na Mwandishi wetu

SERIKALI inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha miundombinu ya Hifadhi za Taifa nchini kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) ikiwemo Hifadhi ya Taifa Ruaha, hatua inayosaidia kuongezeka kwa idadi kubwa ya watalii kwenye Hifadhi hizo.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Mkuu Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Meing’ataki amesema hamasa kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya The Royal Tour imesaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi wanaotembelea Hifadhi hiyo, ambapo uwekezaji wa Mradi wa REGROW utafungua zaidi milango kwa wageni kutalii kwenye Hifadhi hiyo na kuongeza siku za kukaa hifadhini.

Meing’ataki ameongeza kuwa Hifadhi ya Taifa Ruaha ni ya pili kwa ukubwa nchini na iko mbali na mji, Ili wageni wengi waweze kuifurahia ni lazima waweze kuviona vivutio vingi vilivyopo ndani ya Hifadhi hiyo, kwa hiyo pasipokuwa na malazi lengo la kuwaongezea siku za kukaa Hifadhini watalii halitafikiwa, hivyo muda mfupi kuanzia sasa mradi wa REGROW unakwenda kutatua changamoto hiyo.

“Baada ya kukamilika kwa miundombinu hii inayojengwa na mradi wa REGROW, Hifadhi itapokea idadi kubwa sana ya watalii, maana Viwanja vyetu vya ndege vita ruhusu ndege kubwa kubwa kutua na kupokelewa kwenye majengo yetu, kiukweli Mradi huu ni chachu ya Utalii na ongezeko la mapato kupitia sekta ya Utalii” Alisema Meing’ataki,”amesema.

Msimamizi wa Mradi kutoka TANAPA ambaye ndiye anasimamia ujenzi wa Uwanja wa Ndege Hifadhi ya Taifa Ruaha Daniel Malima amesema kiasi cha shilingi Bilioni 17 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo huku Bilioni 42 zikitolewa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Kiganga.

“Mradi wa REGROW umetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya majengo na Kiwanja cha ndege Kiganga uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na Ukwaheri kitakaojengwa upande wa Kusini mwa Hifadhi” Alisema Malima

Aidha Malima ameongeza kuwa kwenye majengo kuna ujenzi wa nyumba za kulala wageni, jengo la kufanya utafiti wa ikolojia, jengo la kupata taarifa za wageni, jengo kwa ajili ya wageni na waongoza utalii pamoja na madereva. Mradi wa REGROW unaotekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia umelenga Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania ambapo kunavivutio likuki vya Utalii huku hadi sasa katika utekelezaji wake watanzania mbalimbali wanaendelea kunufaika kupitia ajira, elimu, Biashara, Kilimo, usalama dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu.