April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhina ahimiza wananchi kutumia nishati ya gesi kupikia

Judith Ferdinand,Timesmajira Online-Mwanza

Wito umetolewa kwa wananchi kutumia nishati ya gesi ya kupikia(LPG) badala ya kutumia nishati chafu kama kuni na mkaa hii itasaidia katika kuimarisha afya zetu pamoja na kutunza mazingira.

Pia nishati ya gesi ni rafiki kwa maana ya gharama yake ni nafuu ukilinganisha na kuni na mkaa.

Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa ,George Mhina hivi karibuni wakati akizungumza na Timesmajira Online ofisini kwake jijini Mwanza.

“Pamoja na kwamba tunasisitiza umuhimu wa kutumia nishati ya gesi lakini tunatoa rai kwamba matumizi yake yafanyike kwa usahihi,tunaponunua gesi tuhakikishe tumeipima uzito wa mitungi,pia usafirishaji wake na haina mivujo,”ameeleza Mhina na kuongeza kuwa:

“Watu waendelee kuhamasika kutumia gesi kwani serikali ina mipango mingi ya kuondoa kodi katika mitungi ya gesi ili kufanya iwe rahisi wananchi kuweza kukitumia,”.

Hata hivyo ameeleza kuwa wameendelea kufuatilia huduma zao katika maeneo ya Kanda ya Ziwa hasa za mafuta ambapo katika kupima vinasaba wamepima vituo vya mafuta takribani 82 ili kujua mafuta yanayotumiwa yamelipiwa kodi kwa maana yamewekewa maka(maker).

“Na katika kuzingatia sheria vituo vyote 82 vilikidhi vigezo hiyo ni katika robo ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi,2024,”.

Pia walipima ubora katika vituo 62 kati ya hivyo vituo viwili ndio vilionekana kuwa mafuta yake hayana ubora ule wa TBS hivyo ni sawa na asilimia 96 vimezingatia viwango vya ubora na katika vituo hivyo viwili ambavyo havijakidhi hatua za kisheria zimechukuliwa ikiwemo ni pamoja na kuvifungia.

Lakini katika sekta ya maji wameona Machi 16 hadi 22, mwaka huu kulikuwa na wiki ya maji walizindua taarifa ya utendaji wa mamlaka za maji Tanzania Bara wameona katika maeneo mengi Kanda ya Ziwa wamefanya vizuri.

Ambapo Mhina ameeleza kuwa Mamlaka kama Biharamulo imekuwa ya kwanza katika kundi lao,Busega ikawa ya tatu katika kundi lao pia ya Maswa imefanya vizuri huku Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira(MWAUWASA),upande wa uondoaji maji taka imefanya vizuri.

“Tumeona kwenye taarifa ile kuwa uzalishaji wa maji umekuwa ukiongezeka hasa takribani Watanzania asilimia 82 wanafikiwa na huduma ya maji, lakini bado tumeona kuna baadhi ya changamoto ambazo tunatakiwa kuzifanyia kazi katika mamlaka zetu za maji ikiwemo kiwango cha upotevu wa maji ambacho kiwango chake ni asilimia 37 nchi nzima,” ameeleza na kuongeza kuwa:

“Maana yake mamlaka zinazalisha maji asilimia 100 lakini asilimia 37 zinapotea kwaio hili ni eneo ambalo mamlaka zinatakiwa zipange na zije na mkakati wa namna gani zinaweza kupambana ili kuondoa uharibifu na upotevu wa maji kwa sababu kiwango cha upotevu kinachokubalika angalau asilimia 20,”.

Hata hivyo ameeleza changamoto nyingine ni mamlaka nyingi hazina mifumo ya kuondoa na kutibu maji taka kwani maji yanayotumika asilimia 80 baadae yanaenda kuwa maji taka.

“Ni mamlaka chache zina mifumo hiyo ingawa taarifa inaonesha zimeongezeka kutoka mamlaka 18 kwa ripoti iliopita hadi 21 bado kiwango ni kidogo kwani nchi nzima kuna mamlaka 85 hivyo inahitaji uwekezaji zaidi,”.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa baadhi ya mamlaka hazina mpango wa biashara ambapo kati ya 85 mamlaka 57 ndio zina mpango huo hivyo eneo hilo bado lina changamoto.

Aidha ameeleza kuwa kumekuwa na mwitikio wa wadau kujitokeza kutuma maombi ya kutaka kuwekeza katika kujenga vituo vya mafuta vijijini ikiwemo Ukerewe, Serengeti na maeneo mengine.