May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchujo Kabaddi kufanyika kabla ya Sept. 30

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

CHAMA cha mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Abdallah Nyoni kimeweka wazi kuwa watahakikisha mambo yote muhimu ikiwemo kufanya mashindano ya Kabaddi kwa ajili ya kufanya mchujo huru wa wachezaji watakaounda timu ya Taifa (Open and fair trial selection at national level) yanatelekezwa kabla ya kumalizika kwa mwezi huu.

Mchujo huo ambao utafanyika jijini Dar es Salaam utasimamiwa na Katibu na Kamati ya Ufundi na uteuzi huo utawahusu wale wote watakaopendekezwa na klabu zao.

Akizungumza na Mtandao huu, Nyoni amesema kuwa watahakikisha yale yote yaliyopangwa kufanyika mwezi huu ndani ya kalenda, yanatekelezwa kwa wakati sahihi ili kuhakikisha mambo yote yanakuwa sawa kabla Desemba ambapo yatafanyika mashindano ya Kabaddi ya Afrika.

Katika mashindano hayo ya Afrika ambayo Tanzania itawakilishwa na timu ya wanaume na wanawake pia zipo timu kutoka nchini Kenya, Cameroon, Egypt, Mauritius, Sirra Leone, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria na Zimbabwe.

Lakini timu za Uingereza, Malaysia, Taiwan, Iraq na India zikionesha nia ya kuja kama waalikwa ingawa ushiriki wao utategemea maamuzi ya bodi ya Kabaddi Afrika (Africa Kabaddi Federation na World Kabaddi).

“Ndani ya kalenda yetu ya matukio kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanya kwa wakati ikiwemo mchujo wa wachezaji wa timu ya Taifa hivyo kama viongozi tutahakikisha mambo haya yanafanyika kabla ya mwezi kuisha,” amesema Nyoni.

Kwa mujibu wa kalenda hiyo, mwezi ujao chama hicho kitaanza kuandaa tathimini na ripoti ya makusanyo ya pesa za kuendesha
mashindano pamoja na kupitia bajeti husika na kuwasafirisha wachezaji wataokwenda kuunga na timu zao za kulipwa nchini India kushiriki ligi ya ‘IIPKL’

Pia wataanza kushughulika vibali vya kuingia nchi kwa wachezaji wa kigeni, kupokea majina ya mwisho kwa wachezaji kwa timu shiriki pamoja na babadiliko ya majina ya wachezaji, viongozi yakiambatana na pasi zao za kusafiria kabla na si chini ya Novemba 30.

Novemba watapokea walimu wa Kabaddi kutoka nchini India
ili kuanza kwa kambi ya timu ya Taifa ya Kabaddi ambapo pia watafanya tathimini ya maandalizi ya mashindano ya Afrika ikiwa pamoja na kuandaa miundombinu ya mashindano (hotel kwa timu, viwanja, chakula na usafiri pamoja na kufanya semina elekezi kwa wanahabari wa Tanzania juu ya kuripoti mchezo wa kabaddi, sheria na kanuni nyingine.

Desemba 8 na 9, 2020 watapokea timu ya wakaguzi na maafisa wa ufundi pamoja na wanahabari toka nje watakaoambatana na maofisa wakuu wa World Kabaddi, Africa Kabaddi Federation na NKIF na Desemba 10 timu zitaanza kuwasili kwa ajili ya mashindano yatakayoanza tarehe 11 hadi 13.