April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Jimbo la Kyela aagiza mradi wa maji ukamilike haraka

Na Cresensia Kapinga, TimesMajira,Online Kyela.

MBUNGE wa Jimbo la Kyela, Ally Mlagila Jumbe, ameitataka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kyela (KASUMULU) kuharakisha ujenzi wa mradi wa maji ambao utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa eneo la Mji Mdogo Kyela kama Serikali ilivyoagiza na si vinginevyo.

Mbunge huyo ametoa agizo hilo leo wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Maji Mbambo-Kyela ambao umefadhiliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Miungano wa Tanzania kwa asilimia 100. Mradi huo utagharimu sh. bilioni 4.7 hadi kukamilika.

Amesema anategemea mradi huu utaendana na viwango vya kimataifa na kitaifa kwa wananchi kupata maji yasioyopungua lita 90 hadi 120 kwa siku kwa kichwa cha mtu.

“Tumekuwa tukizungumza hali ya huduma ya maji leo wanaopata maji safi na salama hapa kwenye mamlaka ni 67,701, lakini wanakuambia ni lita 3,263 ambapo ukigawa kila siku mtu mmoja anapata vindoo viwili vya maji, wakati huo tumetangaza mamlaka hii iendane na viwango vya kimataifa na si vinginevyo,” amesema Mbunge .

Ameeleza kuwa mradi huo mpya ukipiga hesabu ni lita 50 tu kwa idadi ya watu waliyosema, hivyo wakati mwingine wanapeleka miradi mikubwa watu wanakuwa na imani matokeo yake mtu anachota ndoo mbili anaambiwa kalale, hakuna maji, jambo ambalo linakuwa sawa na matusi kwa Serikali.

MBUNGE wa Jimbo la Kyela, Ally Mlaghila Jumbe akifafanua jambo mara baada ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na usafi wa mazingira ambao umefadhiliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kiasi cha sh. Bilioni 4.7. Na mpiga picha wetu.

Aidha amewataka watendaji wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuacha tabia ya kuwakadilia watu kuwa wataenda kuoga mtoni na kunywa watakunywa maji ya bomba na kupikia jambo ambalo kwa sasa halipo hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Isumail Mlawa, aliwataka watendaji wa mamlaka ya maji safi na mazingira Kyela kuandaa mpango kazi ambao utaonesha kwenye mradi huo cha kwanza ni kununua mambomba au kuandaa chanzo ili sasa kazi iweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa na kuharakisha huduma hiyo kwa wakati na si vinginevyo.

” Mradi huu si wetu wala sio wa madiwani huu mradi ni wa wananchi, hakuna sababu ya kuficha mradi huu,nitaomba mpango kazi uandaliwe na tupewe wote hakuna sababu ya kuficha ficha.” Amesema Mkuu wa Wilaya.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KASUMULU, mhandisi Raphael Kolong’onyo amesema mradi huo hadi kukamilika utagharimu kiasi cha sh. Bilioni 4.7 na tayari wameshapokea kiasi cha sh. 800,000,000 na fedha zilizotumika ni kiasi cha sh.478,238,279.76.

Amesema mradi huo unatarajia kuzalisha maji kiasi cha mita za ujazo 1,778 ambapo utawanufaisha zaidi ya wananchi 35,562 na kufanya jumla ya watu wanaopata maji safi na salama kufikia 103,263 sawa na asilimia 83.