April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbio za Mwenge kukagua miradi ya bil.2/- Mtwara

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mtwara

MBIO Maalum za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Mtwara zimeanza kukimbizwa ukitokea Mkoani Lindi huku ukitumika kukagua miradi ya maendeleo saba yenye thamani ya zaidi bilioni 2.

Akitoa salamu kwa kiongozi wa mbio za Mwenge Maalum wa uhuru Kitaifa, Luteni Josephine Mwambashi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dustan Kyobya amesema kuwa, Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Mtwara utakimbizwa kwa umbali wa kilometa 112.3 katika Tarafa sita ambazo ni Mpapura, Mayanga, Mikindani, Mtwara Mjini, Ziwani na Nanyamba, Kata 23, Vijiji 25 na mitaa 44.

Amesema kuwa, mbali na kupita pia Mwenge huo wa uhuru pia utatembelea na kukagua miradi mitano pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi mmoja na kufungua mradi mmoja.

Ujumbe wa Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2021 ni ‘Tehama ni Msingi wa Taifa Endelevu, Itumie kwa Usahihi na Uwajibikaji’ lengo likiwa ni kuelimisha, kuhimiza, kusisitiza na kutafanua kwa wananchi umuhimu wa matumizi sahihi ya Tekinolojia kwa ajili ya shughuli za rushwa.

Kiongozi wa mbio za Mwenge maalum wa uhuru Kitaifa, Luteni Josephine Mwambashi amewataka viongozi wanaopewa dhamana ya kusimamia miradi lazima wawe wazalendo kwa kuwashirikisha wananchi na kuwapa taarifa ya miradi ili wawe na uwezo wa kuridhia miradi yao.

‘Ndugu zangu viongozi mnapopewa dhamana lazima mtoe taarifa ya miradi kwa wananchi kwani inahusu hivyo ni lazima washirikishwe, kuwepo na nyaraka zilizojipanga vizuri ambazo zinaendana na gharama za mradi,”amesema Luteni Mwambashi.

Aidha amebainisha kuwa fedha inayokuja kutoka serikali kuu ni lazima wananchi wapewe taarifa na waambiwe matumizi ya fedha hizo kwa kukaa vikao na wananchi.