May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makumbusho ya Taifa yaja na zao jipya la utalii

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

Makumbusho ya Taifa la Tanzania inatarajia kuwa na programu maalum ya kimakumbusho yenye vionjo vya Kiswahili kama sehemu ya zao jipya la kivutio cha utalii wa utamaduni

Akizungumzia Programu hiyo ya Kimakumbusho itakayofanyika tarehe 6 Agosti 2022, Kijiji Cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amesema jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii nchini hususan kupitia Filamu ya The Royal Tour zinapaswa kuungwa mkono kwa kila namana hivyo wameamua kufanya hivyo kwa kuanzisha zao jipya la utalii ili kutoa fursa kwa watalii wa ndani na nje kufurahia utamaduni wa Kitanzania.

Dkt Lwoga ameongeza kuwa Tanzania ni tajiri wa urithi wa utamaduni ambao Taasisi anayoiongoza kupitia Kijiji cha Makumbusho inahusika katika kuhifadhi na kuipa jamii ya ndani na nje nafasi ya kufurahia uhifadhi ya Urithi huo wa asili hasa kwa kupitia program ya Kiutamaduni.

Aidha, Dkt Lwoga ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kwenye program hiyo itakayopambwa na ngoma ,muziki wenye maadhi ya Pwani, vyakula vya asili, masimulizi, Majigambo pamoja na Mavazi ya asili.