



Na Mwandishi wetu MAELEZO,Dodoma
Serikali imezindua rasmi Mkakati wa Taifa wa miaka 10 unaolenga kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili inayoongezeka kila uchwao na kuacha athari kubwa katika jamii na taifa kwa ujumla.
Mkakati huo wa kuanzia 2026/27 hadi 2036/37 unaashiria dhamira mpya ya kujenga upya maadili, kuimarisha familia, na kulinda utambulisho wa taifa katika zama hizi za mabadiliko makubwa ya teknolojia na kijamii.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Aprili 29, 2026, ukiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Makonda amesema kuwa mmomonyoko wa maadili tayari unaonekana kwa kiwango kikubwa, hasa katika ngazi ya familia na jamii.
Waziri Makonda ameongeza kuwa tatizo hilo linaweza kuonekana si kubwa kwa mtazamo wa juu, lakini uhalisia wake katika familia nyingi ni mbaya na wa kutia wasiwasi.
“Tatizo la mmomonyoko wa maadili linaweza kuonekana sio kubwa lakini kwenye familia zetu hali ni mbaya. Serikali imeandaa mkakati huu ambao ni shirikishi kwa lengo la kujenga jamii yenye utu, uzalendo, mshikamano na uwajibikaji,” amesema Waziri Makonda.
Aidha, amesema licha ya ukiuaji wa teknolojia na matumizi ya mitandao ya kijamii kuongeza urahisi wa upatikanaji wa taarifa pia umechochea kusambaa kwa maudhui hatarishi kama matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya ukatili, lugha chafu, na kudhoofika kwa misingi ya familia.
Kufuatia hali hiyo Waziri Makonda amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti ili kulinda maadili ya jamii kuendana na utamaduni wa Kitanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa utekelezaji wa mkakati huo utawezesha taifa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga jamii yenye maadili mema, nidhamu na rasilimali watu bora kwa maendeleo endelevu.
Awali ,Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema changamoto kubwa si kuandaa sera bali ni kuhakikisha utekelezaji wake hivyo akesema Serikali imejipanga kikamilifu kusimamia utekelezaji wa mkakati huo unaleta matokeo halisi kwa jamii na Taifa.

More Stories
Mradi wa maji Nkasi suluhisho la afya kwa jamii
Tanzania yahimizwa kukomesha adhabu za viboko
Tanzania shule ya Utumishi Barani Afrika