April 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yahimizwa kukomesha adhabu za viboko

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKATI Tanzania ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu za Viboko, inayoadhimishwa duniani, Aprili 30, mashirika ya haki za watoto na washirika wa asasi za kiraia wametoa wito wa pamoja wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha adhabu za viboko na kulinda watoto dhidi ya aina zote za ukatili katika mazingitra ya kujifunzia.

Wito huo umetolewa leo katika mkutano na waandishi wa habari na Kikundi Kazi cha Kisekta cha Kukomesha Adhabu za Viboko nchini Tanzania.

Kikundi hicho kinajumuisha Save the Children/Tanzania, Women in Law and Development inAfrica (WiLDAF), UNICEF, World Health Organization (WHO), HakiElimu, Zanzibar Children Right Forum (ZCRF), Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA).

Vingine ni Shule Direct, Child Dignity Forum (CDF), Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Msichana Initiative, Legal and Human Rights Centre (LHRC), FAWE Tanzania, ZAPHA+ , Zanzibar Legal Aid and Human Rights Organization (ZALHO), Tanzania Media Women Association (TAMWA), na Christian Social Services Commission (CSSC).

Kwa pamoja, wameeleza kuwa adhabu za viboko bado ni miongoni mwa aina za ukatili dhidi ya watoto zilizoenea zaidi na kukubalika kijamii nchini Tanzania.

Adhabu za viboko, ikiwemo kupiga kwa fimbo, kupiga makofi na kudhalilisha kwa maneno, zinaendelea kuwaathiri watoto shuleni, madrasa, majumbani na katika mazingira mengine ya kujifunzia.

Licha ya kuenea kwake, ushahidi unaonyesha wazi kuwa adhabu hizo haziboresha nidhamu wala matokeo ya elimu. Duniani kote, karibu watoto watatu kati ya wanne wenye umri wa miaka 2–14 hupitia nidhamu ya ukatili majumbani.

Nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 70 ya watoto hupitia ukatili wa kimwili katika utoto wao, huku walimu wakiwa miongoni mwa wahusika wanaoripotiwa mara nyingi katika mazingira ya shule.

Tafiti zinaonyesha kuwa adhabu za viboko husababisha hofu, kujitenga, kupungua kwa ushiriki, kushuka kwa ufaulu wa masomo, pamoja na madhara ya muda mrefu ya kihisia na kisaikolojia.

“Adhabu za viboko zinadhoofisha utu wa mtoto na uwezo wake wa kujifunza na kufanikiwa,” amesema Kauleni, Mkurugenzi wa Nchi wa Save the Children Tanzania na Mwenyekiti wa muungano huo.

Ameongeza: “Kuzikomesha ni hatua muhimu katika kujenga mazingira salama, jumuishi na yenye ufanisi ya kujifunzia kwa kila mtoto.”

Naye Mkuu wa Ulinzi wa Mtoto wa UNICEF Tanzania, Miranda Armstrong, ameongeza:

“Ukatili hauna nafasi katika elimu. Ushahidi uko wazi, adhabu za viboko zinaumiza watoto na haziboresha nidhamu. Kinachohitajika sasa ni hatua madhubuti.”

Tanzania imeonyesha dhamira kubwa ya kulinda watoto kwa kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto, pamoja na kuwa nchi kinara chini ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Kukomesha Ukatili Dhidi ya Watoto.