April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makinda: vijana tumieni takwimu za sensa kama fursa ya kujiinua kiuchumi

Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi,Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda,amewahimiza vijana na jamii nchini kutumia matokeo ya takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kama fursa ya kuangalia masoko ya shughuli za kiuchumi wanazofanya.

Ikiwa ni pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kufanya biashara na kufikia masoko hayo pia takwimu hizo ziwafumbue macho watendaji wa serikali katika kupanga mipango wezeshi kwa vijana ili kujikwamua kiuchumi.

Makinda ameeleza hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu katika mkutano wa tathmini ya zoezi la sensa uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Buswelu katika ziara yake wilayani Ilemela yenye lengo la kuwashukuru watanzania kwa namna walivyoweza kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi mwaka 2022.

Ambapo ameeleza kuwa sensa ya anuani na makazi iliyofanyika mwaka jana moja ya lengo ni kurahisisha mawasiliano na kutoa urahisi wa watu kufikiwa katika makazi yao,hivyo ni fursa kwa vijana kufanya biashara kwa njia ya mtandao kwa kuweza kuagiza bidhaa nje ya nchi na kumfikia nyumbani kwake bila kwenda nchi husika.

“Hizi simu zenu za kiganjani ni ajira hata kama mama ntilie ukijua kufungua hiyo simu unafundishwa kupika mapishi ya aina yoyote,biashara leo siyo lazima upande ndege kwenda china unafanya biashara ukiwa na simu yako bahati mbaya wenzetu wanakaa usiku wanaangalia mambo ya ovyo ovyo tu ambayo tunakataa,fanyeni biashara kimtandao ndio maana tumefanya sensa ya anuani za makazi ambayo unaweza kufanya biashara na dunia popote pale bila kuhitajika kwenda nje ya nchi,”ameeleza Makinda.

Pia ameeleza kuwa takwimu ni fursa siyo kwa serikali tu hata kwa mwananchi mmoja mmoja,ambapo ukitaka kufanya biashara zitakuambia soko lako lilipo ambapo utajua kabisa eneo fulani lina idadi ya watu wengi zaidi hivyo unaenda kufanya biashara huko huko.

“Rais akasema wakati wa sensa hii ifanyike na ya anuani za makazi na majengo,ambayo hayakuhesabiwa kwa sababu ya kodi tu, ila ina rahisisha leo hii nikitaka kufika mahali nikiingia tu kwenye mtandao nafika mpaka eneo husika ninalohitaji kufika,”ameeleza Makinda.

Pia ametumia fursa hiyo kuwaeleza vijana kuacha tabia ya kuchagua kazi bali kupitia sensa hiyo wakafumbuliwe macho na kuachana na mawazo potofu kuwa kwa sababu ni msomi lazima afanye kazi fulani.

“Kazi zinazoendana na kisomo ulichosoma hazipo wakati sisi tunasoma tulikuwa tunasema elimu ni msingi wa maisha lakini siyo msingi wa ajira,ndio maana tunasema sensa yetu hii ikufumbue wewe uliosoma,fursa za ajira zipo nyingi leo tunajenga SGR na vitu vingine tatizo ni vijana kuchagua kazi na ukichagua kazi hakika hautapata mpaka utazee ‘utastaafu kabla ya kuajiriwa,”ameeleza Makinda.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kata ya Buswelu waliohudhuria mkutano huo,wameomba elimu ya sensa isiwe inasubilia mpaka kipindi cha zoezi la kuhesabiwa bali ipelekwe shuleni watoto wafundishwe ili wake wakielewa maana ya sensa.

Pia serikali iondoe kampuni za mchezo wa kubahatisha ili vijana waamini katika kufanya kazi na siyo kama ilivyo sasa wanaamini katika bahati.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Anne Makinda, akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu hawapo pichani wakati wa mkutano wa tathmini ya zoezi la sensa uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Buswelu katika ziara yake wilayani Ilemela yenye lengo la kuwashukuru watanzania kwa namna walivyoweza kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi mwaka 2022.
ItBaadhi ya wananchi wa Kata ya Buswelu waliohudhuria wa mkutano wa tathmini ya zoezi la sensa uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Buswelu katika ziara yake wilayani Ilemela yenye lengo la kuwashukuru watanzania kwa namna walivyoweza kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi mwaka 2022