May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubalozi wa China wakabidhi vyerehani, mashine za kutotolea vifaranga

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

UBALOZI wa China nchini wamekabidhi vyerehani 425 na Mashine za kutotolesha vifaranga 250 vyenye thamani ya shilingi Milioni 79 kwa wanawake wajasiriamali wa kitanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Waziri Wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kuendelea kudumisha mahusianao mema na China, yakiwepo kujifunza namna wanawake wa China walivyoweza kufanikiwa kiuchumi na kisiasa.

“Tutahakikisha vifaa hivyo vinawafikia walengwa kwa wakati husika. Natambua China ni nchi iliyoendelea. Hivyo, Mataifa yetu ni muhimu kuweka mipango ambayo itawanufaisha zaidi wanawake wajasiriamali wa Tanzania wakaja China na wa China kuja Tanzania kujionea jinsi wanawake wa pande zote mbili wanavyoshiriki katika shughuli za kiuchumi na kisiasa na mbinu wanazotumia katika kupata mafanikio kwa nyanja mbalimbali.”

Aidha, alibainisha kwamba Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya wanawake ya mwaka 2023 inayotoa kipaumbele kuwezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuondoa ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini, Chen Mingian alibainisha kuwa, kwa kipindi alichofanya kazi Tanzania amejionea Rais Samia Suluhu Hassan akitilia mkazo masuala yanayohusu wanawake na kushuhudia baadhi ya wanawake wenye uwezo mkubwa.

Aliongeza kwamba Ubalozi wa China hivi umekuwa ukitoa misaada mbalimbali ya kuwanufaisha wanawake kwenye maeneo tofauti nchini kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi, hivyo msaada huo anaamini utawasaidia walengwa kuongeza kipato.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya wanawake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi, Mary Chatanda, aliushukuru Ubalozi wa China kwa kuikumbuka CWT kama sehemu ya wanufaika hivyo hawana budi kuendeleza mradi huo kama jukumu la msingi kwa ustawi mkubwa ili kuwa na uchumi imara.