May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAEC yaongeza ukusanyaji maduhuli uongozi wa Samia

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

TUME ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), imeongeza makusanya ya maduhuli ya Serikali kutoka sh.bilioni 8.7 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia sh. bilioni 10.9 mwaka wa fedha 2022/2023 kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yalisema leo jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof.Lazaro Busagala wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika Mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema, mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufungua ofisi za kanda, mipakani na kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Hii imechangiwa na serikali kutengeneza mifumo ya TEHAMA, lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi,” amesema Prof. Busagala.

Ameitaja mifumo hiyo kuwa ni pamojaa na mfumo wa malipo ya Leseni na na Forodha (TANCIS), mifumo ya Kielektronic pamoja na Uondoshaji wa Shehena Bandarini na maeneo mengine ya forodha (TeSWAS) na mfumo wa Kielektronic wa nyaraka (EDMS) katika kutoa huduma.

Katika hatua nyingine, Prof. Busagala ametaja baadhi ya mafanikio ya TAEC waliyoyapata chini uongozi wa Rais Dkt. Samia kuwa ni pamoja na kusogeza huduma kwa kujenga ofisi katika Kanda

“Serikali imeendelea kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga miundo mbinu inayoipa TAEC uwezo wa kutoa huduma kwa tija na ufanisi.

Serikali imejenga majengo sita ya maaabara na ofisi katika kanda 5 yenye thamani ya takribani Bilion 28. 11 ambapo majengo manne kati ya hayo yamekamilika. Miradi hiyo ipo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar,” amesema Prof. Busagala.

Aidha, amesema mafanikio mengine ni Kupunguza siku za utoaji wa cheti cha uchunguzi wa mionzi (RAC) kutoka zaidi ya siku saba hadi kufikia kwa wastani wa saa 3 hadi siku moja kwa asilimia 98.

Ameongeza kuwa, awali utaratibu wa RAC ulikuwa una mlolongo mrefu ambao ulisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali, hivyo mfumo wa kielektronic: rac.taec.go.tz umesaidia sana.

Mbali na hivyo pia, amesema Serikali ya awamu ya sita imeondoa tozo na kupunguza tozo kwa kuamua kubeba gharama za upimaji (subsidy)

“Hiii ni hasa kwa wale wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kwa kupunguza kutoka asilimia 0.2 ya malipwani kuwa asilimia 0.1 ya malipwani, sawa na punguzo la asilimia 50.

“Kwa wafanyabiashara wadogo hupatiwa huduma ya upimaji wa sampuli bure sawa na punguzo la asilimia 100,” amesema.

Vilevile, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweza kuongeza idadi ya watumishi wa kudumu kutoka 89 hadi kufikia 142. Kwa kufanya hivyo, TAEC imeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwahudumia wananchi kwa uharaka zaidi.

Lakini pia, Serikali imetatua tatizo la watumishi wa TAEC kupandishwa vyeo baadhi ya watumishi lililodumu kwa muda mrefu. Alisema watumishi 57 wa TAEC walikuwa na matatizo yaliyodumu kwa muda mrefu lakini Serikali ya awamu ya sita imeyatatua

Mbali na hivyo, pia amesema, Serikali ya Awamu Sita kupitia TAEC ipo katika hatua za mwisho kukamalisha mpango wa ufadhili kwa vijana wa kitanzania kusoma vyuo vya nje ya nchi masomo ya teknolojia na sayansi ya nyuklia katika ngazi ya shahada za uzamili

“Kila mwaka vijana watano watapata ufadhili huu. Lengo la ufadhili huu ni kuongeza idadi ya wataalam nchini katika nyanja ya teknolojia na sayansi ya nyuklia ili kuhakikisha kwamba nchi inanufaika ipasavyo na fursa za sayansi ya nyuklia,” amesema Prof. Busagala.

Aidha, amesema, Serikali kupitia TAEC, imebuni na kutengeneza trela maalum la kubebea vyanzo vya mionzi. Alisema, awali watumishi na vyanzo vya mionzi walikuwa wanakaa kwenye gari moja linalotenganishwa na vifaa ambavyo havizuii sawasawa mionzi.

“Jambo hili lilikuwa linahatarisha usalama wa watumishi wanao safirisha vyanzo vya mionzi, wananchi pamoja na mazingira kwa ujumla,” amesema.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TAEC imeendelea na juhudi za kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyukilia nchini.

Aidha, alisema TAEC imefanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanaelewa fursa zilizopo katika matumizi salama ya sayansi ya nyuklia kwa ajili ya kujilitea maendeleo.

Pia amesema, TAEC imeongeza program za kujitangaza kutoka 12 hadi 60 kwenye TV, Redio, magazeti, mitandao ya kijamii na kushiriki katika maonesho mbalimbali.

Prof. Busagala amesema, mafanikio mengine ni, Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuongeza tengeo la bajeti ya utafiti kwa TAEC hadi kufikia Tsh 450M katika mwaka wa fedha 2023/2024.

“Juhudi hizi zimefanyika ili kupata fursa zaidi za sayansi na teknolojia ya nyukilia na pia kuwalinda wananchi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi,” alisema.

Amesema, Katika miaka mitatu machapisho 25 yakitafiti yamepatikana katika juhudi hizi. Pia, alisema Vifaa vya kisayansi ni nguzo muhimu katika kudhibiti athari za mionzi, tafiti, usimamizi na uendelezaji wa Teknolojia ya Nyuklia.

Hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka bajeti na kununua vifaa. Vifaa vya jumla ya TSh. 2.9 Billion vinaendelea kununuliwa. Akizungumzia mipango iliyopo kwa sasa, Prof. Busagala alisema Serikali ina mpango wa Kusimika Kinu cha Utafiti cha Nyuklia.

“Kinu cha utafiti cha nyuklia (Nuclear Research Reactor) ni muhimu sana kwa ajili ya utafiti, kufundishia na kuweka mazingira ya kuwa na viwanda vya madawa ya kutibu saratani (radio-pharmaceautical industries).

“Vinu vingi vya nyuklia duniani vya namna hii hutumika kwa utafiti na mafunzo, majaribio ya ubora wa vifaa, au utengenezaji wa isotopu za dawa.

“Kwa sasa, vyuo vikuu hazina aina hii ya vinu na baadhi ya tafiti haziwezi kufanyika kwa sababu ya kutokuwa na kinu cha utafiti cha nyuklia,” amesema Prof. Busagala.

Ameipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwa mafaniko makubwa iliyopata katika Nyanja ya Teknolojia na Sayansi ya Nyuklia.

Amesema, maono na maelekezo ya Rais pamoja na Usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Nyukilia na Bodi ya TAEC yameiwezesha TAEC kutekeleza Sera ya Taifa ya Sayansi ya Nyuklia kikamilifu.