May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi awafunda wanafunzi St. Mary’s Mazinde Juu

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaasa wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana St. Mary’s Mazinde Juu kusoma kwa kujiamini huku wakizingatia ndoto zao za kuwa wanataka kuwa nani kwenye maisha yao.

Amesema kusoma shule hiyo ni fursa kwenye maisha, sababu watafundishwa mambo mengi ikiwemo taaluma, maadili, nidhamu pamoja na utulivu wanaopata, hivyo wanatakiwa kusoma kwa kujiamini, huku wakiwa wamebeba ndoto kwenye maisha ili kujisaidia wao,familia,jamii na taifa.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza na sita shule ya sekondari ya wasichana St. Mary’s Mazinde Juu.

Mhandisi Mahindi ameyasema hayo alipotembelea shule hiyo ambayo alisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1995 hadi 1999, na kwenda kumalizia kidato cha sita Makongo High School jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine amewapa zawadi ya taulo za kike, biskuti na pipi wanafunzi wa shule hiyo.

“Tunataka kuona viongozi wa kesho wanatoka hapa,Mawaziri wanatoka hapa, wakuu wa mikoa, wahandisi na wataalamu wengine,mimi nilipambana kuona ninakuwa kiongozi hata nilivyokuwa hapa, nilikuwa Dada Mkuu, hivyo na ninyi mnatakiwa kuwa na ndoto kwa kila jambo mnalofanya,”amesema Mahundi.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (kushoto) akikabidhi zawadi za taulo za kike, biskuti na pipi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana St. Mary’s Mazinde Juu iliyopo Magamba, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Mkuu wa Shule hiyo ambayo inaendeshwa na Masista wa Shirika la Mama wa Usambara (COLU) chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Mtawa Evetha Kilamba, amemshukuru Naibu Waziri kwa zawadi alizowapelekea, lakini kikubwa kuweza kuwakumbuka na kufika shuleni hapo baada ya kupita miaka 26 tangu kusoma shule hiyo.

Dada Mkuu (mstaafu) ambaye pia anasoma kidato cha sita kwenye shule hiyo Margareth Mboya, amesema kuwa huo ni upendo mkubwa, na wao wataendelea kuthamini zawadi hizo, na kumtakia kila la kheri Naibu Waziri kwenye majukumu yake ya kila siku.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akibarikiwa na Meneja na muanzilishi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Mary’s Mazinde Juu Padre Damian Milliken (OSB),
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akisalimiana na Mtawa Christiana Mduma (katikati) ambaye wamesoma wote kwenye shule ya sekondari ya wasichana St. Mary’s Mazinde Juu miaka 26 iliyopita. Kulia ni Mkuu wa Shule hiyo, Mtawa Evetha Kilamba.
Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana St. Mary’s Mazinde Juu, Mtawa Evetha Kilamba akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo (hawapo pichani), baada ya kumpokea Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa pili kushoto). wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro (kulia) na Meneja na muanzilishi wa shule hiyo mwaka 1989, Padre Damian Milliken (OSB) (kushoto).