April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuf Ngenya, akikagua bidhaa za wazalishaji waliopatiwa leseni na vyeti vya kutumia alama ya ubora ya shirika hilo hivi karibuni, makao makuu ya shirika, Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Mafunzo ya viwango yanavyochochea mabadiliko chanya kwa wazalishaji

Na Penina Malundo

VIWANGO ni nyenzo madhubuti ya kuongoza mabadiliko na kuainisha njia zinazoweza kufungua masoko na kujenga mazingira mazuri ya kibiashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa lugha nyepesi, viwango huchochea ukuaji wa haraka wa uchumi na ni nyenzo muhimu inayotumika katika uwezeshaji wa biashara na kuleta ukuaji wa uchumi ulio sawia ndani ya jamii.

Msingi huo ndiyo unaowasukuma wataalamu kujitolea ujuzi wao kwa maslahi ya umma kwa kukutana na kutayarisha viwango ambavyo husambaza ubunifu na uvumbuzi katika nchi zao, hivyo kuweka jukwaa la mabadiliko chanya kwa taasisi za biashara, Serikali na jamii kwa ujumla.

Kwa Tanzania, jukumu la kusimamia viwango lipo chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Shirika hilo ambalo lipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Moja ya majukumu ya shirika hili ni kueneza uelewa na kukuza matumizi ya viwango na kanuni za udhibiti wa ubora katika sekta za viwanda na biashara, kwa nia ya kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuzalisha bidhaa bora zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Lengo la hatua hiyo ni kukuza uwepo wa bidhaa na huduma bora na salama kwa umma wa Watanzania na kuchochea maendeleo ya Taifa kiuchumi.

Kwa umuhimu huo, TBS imekuwa ikifikisha mafunzo kwa wadau wanaotaka kupata huduma zinazotolewa shirika na maelekezo mengine kupitia Kitengo cha Utafiti na Mafunzo.

Meneja wa Utafiti na Mafunzo wa TBS, Hamis Sudi Mwanasala, anasema mafunzo yanayotolewa ni ya namna tatu tofauti au zaidi. Mafunzo hayo ni yale yanayotokana na viwango vya mifumo (Management Syestem Standards)

Anasema kuna mafunzo ya kwa ajili ya kuwaelimisha wajasiriamali ambao wamepitia SIDO, wafanyabiashara na kwingineko ambako taasisi zimewasajili ili wazalishe bidhaa, lakini mwisho wa siku kutokana na ushindani wa biashara lazima waende TBS kwa ajili ya kufuata utaratibu ili waweze kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili ziongezwe thamani, lakini vile vile ziweze kuwapatia wajasiriamali na wafanyabiashara masoko ndani na nje ta nchi.

“Kwa maana hiyo kwa kufanya hivyo tunakuwa tumewaongezea imani kwa wateja wao pale zinapoonekana zimethibitishwa na TBS na hivyo hata walaji wanakuwa na uhakika na usalama wa afya zao.” Anasema Sudi.

Anasema kujiamini kwa walaji kunaongezeka kwani wananunua bidhaa ambayo wana uhakika nayo kwa afya na usalama wao, lakini pili inaenda sambamba na thamani ya hela wanayotoa.

“Kwa hiyo iwapo utanunua fungu la nyanya labda kwa sh. 200 halafu baadaye ukapata matatizo ya tumbo ukatumia hela nyingi kujitibu, wakati kumbe kama ingethibitishwa gharama hizo zisingetokea,”Anasema Sudi na kuongeza’

“Kwa hiyo haina maana kununua bati ambayo haina kiwango ndani miaka miwili ikawa imeshika kutu. Lakini kama ungetoa hela ukanunua ambayo imethibitishwa ungeweza kuepukana nayo ukanunua bati ambayo ingekaa muda mrefu.”

Anataja mafunzo mengine kuwa ni kutia mafunzo kwa ujumla wake, hapo akiunganisha na mafunzo ambayo yanayotoka kwa maombi ya makundi mbalimbali.

“Kwa mfano watu wanasema sisi Bodi ya Mawaziwa tunataka watu wetu wanaozalisha maziwa wapate uelewa wa uzalishaji bora wa maziwa hatimaye wathibitishiwe ubora wa maziwa yao, lakini pengine hiyo haipo kwenye programu yetu ya kila mwaka, wakija kwetu tunawapatia mafunzo,” anasema Sudi na kuongeza;

“Wakunaja watunzaji wa mafuta ya kupikia, pengine chama cha wazalishaji wa mafuta ya alizeti ambao wamekuwa wakianika tu juani na wakati wote wanakamuakamua, mwisho wa siku kazi wanayofanya ni kubwa na kipato hawakipati, magari yanakuja kama wateja, wanaangalia na kuondoka wanakwamba wapi? Hayana ubora, wateja wanataka TBS, nao tunataka wabadilike kupitia mafunzo.”

Vile vile, Sudi anasema viwandani pale wanapohitajika wanatoa mafunzo ambayo ni ya kwenye uzalishaji kwa ajili ya kutoa tafsiri ya viwango.

Anasema pale wanapopelekewa maombi kwa ajili ya kufundisha wanafanya hivyo na kwamba imeishawahi kutokea kuna watu ambao wanatengeneza vilainishi vya mitambo, waliomba kupatiwa mafunzo.

Pia anasema kuna watu ambao shughuli zao ni uondoaji wa mizigo bandarini, nao walipatiwa mafunzo na uelewa na wajasiriamali wamepewa maafunzo mengi karibu kila mwaka.

“Sasa hivi tunapata watu ambao ni kundi la watu wenye ulemavu wa kutosikia (viziwi) kuna Tanga na Kigoma wanataka mafunzo na tunajipanga kwenda kupeleka mafunzo hayo huko.

Kwenye kufundisha mafunzo ya kwenye mifumo ya viwango (System Standards) Sudi anasema kuna viwango kama vya aina nne au tano.

Anasema kuna kiwango cha ISO 9714015, ambacho matakwa yaliyoainishwa humo ndani taasisi inaweza kuanza na watu wawili au zaidi wanafuata utaratibu uliomo humo ndani ya kuendesha kampuni ili iwe na tija katika uzalishaji wake, inatoa huduma bora, lakini kwa haraka na inaondoa ukiritimba.

“Lakini pia kila mshiriki katika kampuni au taasisi husika anakuwa na umuhimu wake.

Anasema kunakuwa na menejimeti ya juu katika kutoa maamuzi, lakini kunakuwa na utaratibu wa kujifanyia tathimini ili kujua wapi wamekwama, wamekosea nini ili mwisho wa siku waone huduma zile katika hiyo kampuni wanatoa huduma zinakididhi kile ambacho kinatarajiwa na wateja.” anasema.

Anasema kiwango kingine kwenye huo mfumo ni kuhusu masuala ya mazingira ISO 140001.

Kwa mujibu wa Sudi, hiyi inasaidia makampuni mfano Twiga Cement kwamba matakwa matakwaa wakiwafuata katika uzalishaji wao mazingira yatakuwa salama na wakati mwingine hatua hiyo inaleta picha nzuri kwa wale wanaopata huduma (wateja).

Vinginevyo, anasema uzalishaji usiozingatia utunzaji mazingira unaweza kuleta picha mbaya na kampuni husika kujikuta ikitumia nguvu kuondoa uchafu kwa sababu ya kutojua utaratibu wa kufuata ili mazingira yawe mazuri.

Anataja kazi nyingine za kitengo hicho ni husiana na masuala ya afya na usalama sehemu za kazi.

“Unazalisha sawa lakini usafi wako ukoje? unachokizalisha kama ni mafuta, mkate usafi wake ukoje? Kwa hiyo mzalishaji anatakiwa kufahamu jengo analotakiwa kulitumia kuzalisha bidhaa zake liwe vipi, mfumo wa hewa uwe vipi,” anasema Sudi.

Anasema viwanda vinatakiwa kuwa sehemu ya kudhibiti vihatari kwenye bidhaa zinazozalishwa ili kuhakikisha kitu kinapotoka sehemu moja kwenye nyingine, mfano eneo la kusagia na kikifika sehemu ya kuchanganywa labda maji katika kila hatua ya uzalishaji kusiwe na vihatarishi vinavyoweza kuingia kwenye bidhaa inayozalishwa.

Kwa msingi huo anasema ni muhimu kila sehemu ya uzalishaji kukawa na ufuatiliaji na kila malighafi ikajulikana imezalishwa siku gani, hivyo inakuwa ni rahisi kutambua sehemu yenye matatizo pindi yanapojitokeza.

Anatoa mfano kwamba kama mifumo ya uzalishaji inaposhindwa kutambua kuwa malighafi fulani hazina ubora, mwisho wa siku kile kitakachozalishwa hakitakuwa na ubora.

Kwa mujibu wa Sudi unapokuwa na mfumo huo mzuri inakuwa rahisi kufuatilia malighafi yenye matatizo

Kwa msingi huo anasema mafunzo uthibitishaji wa mifumo unamsaidia mzalishaji au mtoaji wa huduma kufuata taratibu ambazo zitamwezesha kufikia malengo yake.

“Kwa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo kipo kwa ajili ya kuwapa watu uelewa kuhusu kiwango matakwa yanayohitajika ili mwisho wa siku mzalishaji aweze kuambiwa mifumo yake inafuata kiwango husika,”anasema.

Kwa mujibu wa Sudi jambo ambalo TBS inajivunia ni kuongezeka idadi wanaoomba kuthibitishiwa bidhaa zao (Certification) na kwamba wengi wametokana na mafunzo yanayotolewa na kitengo hicho.

“Katika kitengo chetu mafunzo ni kitu ambacho tunajivunia ni kuwa tunapotoa mafunzo kwa walengwe wa kada mbalimbali, baada ya mafunzo tunarudi tena kwa walengwa hao ili kuangalia matokeo,” anasema……….. na kusisitiza;

“Tunafanya hivyo ili kujiridhisha kama hayo mafunzo yameleta tija na mara nyingi tumejiridhisha kwamba wengi wanajitokeza sana kuomba kupata Certification wengi wao ni wale waliotokana na mafunzo ambayo tumewapatia.”

Kwa msingi huo anasema mafunzo ni kitu ambacho ni cha kujivunia na kuahidi kwamba yataendelea kuwa ni endelevu ikiwa ni sehemu ya mifumo ya shirika hilo kila siku.

Sudi anazidi kuongeza kwamba mafunzo hayo yanasaidia sana na kuwa kwa sasa wapo kwenye programu ya kufundisha wajasiriamali. Anazidi kueleza kwamba hawaishii kwenye mafunzo peke yake bali wanaenda mbali zaidi kwa kufanya tathmini ili kujua matokeo ya mafunzo akitoa mfano kwamba wamefanya Bukoba, Geita na Mwanza.

Anasema Bukoba walienda Januari, mwaka huu ambapo walifundisha watu 117 na mwezi uliopita (Julai) walirudi tena kwa ajili ya kufanya tathmini ya matokeo, kwani baada ya watu hao kufundisha na kupata uelewa walituma maombi ya kupata leseni ya kutumia nembo ya TBS.

“Watu 70 au 80 hivi walileta wameomba kati yao 10 au 15 wamefanikia kabisa kupata alama ya ubora baada ya kukidhi vigezo, lakini wengine kuna maeneo hayakwenda vizuri wanayafanyia masahihisho,” anafafanua Sudi.

Kwa wale ambao wanashindwa, Sudi anasema wanarudia kuwaelimisha. “Hawa watu wakishapata alama ya ubora ya TBS wanakuwa na tija kwa Serikali, kwani uuzaji bidhaa zao unaongeze kwenye masoko na maana yake wanalipa kodi na fedha zinazopatikana zinaenda kutengeneza miradi ya maendeleo ikiwemo shule na hospitali.

Pia anasema wanapotoa mafunzo ni lazima watu waambiwe kuwa kiwango fulani ni cha lazima, hivyo ni muhimu wakifuate na wasipofanya hivyo madhara ya kukiuka masharti yake ni nini.

Hivyo anasema ndiyo maana kumekuwa wakitoka nje kwa ajili ya kutoa mafunzo ili wananchi waweze kuelewa.

Anasema bila wao kutoka nje kwenda kufundisha ni vigumu watu kuelewa, hivyo wao ndiyo wenye jukumu la kuwaambia watu ili wajue ndiyo maana kwa makusudi kumekuwa na kitengo cha mafunzo.