April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madereva wa mabasi wanaendesha kwa mwendo kasi waonywa

Na Nasra Bakari, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MKUU wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Adam Maro amewataka madereva kuacha tabia ya kuendesha mabasi kwa mwendo kasi kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumza jana na madereva wa mabasi yanayofanya safari zake toka Mkoa wa Arusha kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania Maro alisema, katika kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kama siyo kuisha kabisa Jeshi la Polisi kimeendesha operesheni  ya ukaguzi wa mabasi yanayobeba abiri katika stendi ya mkoa huo na kutoa elimu kwa madereva.

“Pia nawaasa kufanya ukaguzi wa vyombo vyao kabla ya kuanza safari ili kuepusha madhara ya ajali ambayo yanaweza kutokea kutokana na ubovu wa magari hayo,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Solomon Mwangamilo alisema, akiwa ni msimamizi wa sheria za usalama barabarani katika  mkoa wake hatakua na huruma wala kumuonea muhali dereva yeyote ambaye  atafanya uzembe barabarani.

Naye Katibu wa Chama cha Kutetea abiria Kanda ya Kaskazini Godwin Mpinga alisema, taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na jeshi la polisi kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara za madereva wanaokiuka sheria za barabarani.

Aidha George Joseph ambaye ni dereva ametoa wito kwa wenzake kuhakikisha wanaendesha kwa kufuata sheria na kuacha tabia ya kusikiliza wachache wanaowashinikiza kutembea mwendokasi kwa lengo la kuwahi.