April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Machinga wavamia kanisa

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online

Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama Wamachinga jijini Dar es Salaam waliopo eneo la Mbuyuni Kata ya Wazo Wilaya ya Kinondoni, wamevamia eneo la Kanisa la Orthodox na kuanza kufanya biashara jambo ambalo limelalamikiwa na uongozi wa kanisa hilo.

Kundi hilo la wamchinga zaidi ya 200 wamevamia eneo hilo la kanisa wakidai kuwa ni la wazi linamilikiwa na Serikali hivyo wanaenda hapo kufanya biashara zao baada ya kufukuzwa barabarani.

Wakizungumzia tukio hilo, Makamu wa Askofu wa Kanisa hilo jimbo la Dar es Salaam, Cleophace Bachuba amesema kuvamia kwa wamachinga hao katika eneo lao kimesababisha baadhi ya shughuli za kanisa kusimama.

Amesema tayari wameshatoa taarifa kwa uongozi wa Serikali za mtaa na Wilaya ambao uliwarudishia majibu kuwa hilo sio eneo la wafanyabiashara hivyo wavamizi wanapaswa kuondoka kupisha shughuli za kanisa kuendelea.

“Wakati Serikali inafanya oparesheni ya kuwaondoa wamachinga barabarani ndipo hawa wa eneo la Mbuyuni wakavamia eneo letu hili la kanisa na kukwamisha shughuli zingine kuweza kuendelea,” amesema na kuongeza

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopanga wamachinga ili wakae vizuri ili wajipatie liziki zao, sisi wote ni jamii moja ya watanzania, kwa upande wetu tunafanya kazi na wananchi hatupaswi kugombana, kuchukiana wala kusali kwa shida, hivyo tunaomba serikali itusaidie katika hili,” amesema

Naye Paroko wa Kanisa hilo, Padri Frumentios Msuri alisema kanisa hilo la Bikiria la Maria lilijengwa mwaka 1939 na tangu hapo watanzania, wagiliki na watu wa aina mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusali lakini baada ya virugu hizo wamelazimika kusali Upanga.

“Tangu lililopojengwa tumekuwepo hapa licha ya eneo letu kumegwamegwa, leo na hawa machinga wanataka kuvamia, tunaomba Serikali ituangalie na iwapangie eneo la kwenda ndugu zetu hawa ambao wanatafuta riziki kwa ajili ya familia zao,” amesema

Kwa upande wake mwenyekiti wa wamachinga hao, Kizito Ponsiano amesema wafanyabishara hao hawafanyi biashara zao katika eneo la kanisa na kusisitiza kuwa eneo hilo sio lote ni mali ya kanisa.

Hata hivyo alisema wanauomba uongozi wa kanisa hilo kuwapatia vielelezo vinavyoonesha kuwa eneo hilo ni mali yao na kwamba wakiviona na kujiridhisha wataondoka na kutafuta eneo lingine.

Akijibu madai hayo, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Mbuyuni Salasala, Robart Masawe alisema katika eneo lake wafanyabiashara wamepangiwa eneo la Benako ambalo lina mgogoro na eneo la Kisanga ambalo halina choo kwa sasa.

“Diwani anapambana sasa hivi ili kupatikane choo, tukimaliza kujenga wamachinga hawa watatolewa na kwenda kupangwa katika eneo hilo wala hakuna tatizo,” amesema

Hata hivyo Masawa amesema eneo waliopo wafanyabiashara hao limejitenga kabisa na kaanisa hilo, na kuongeza kuwa mgogoro huo ulipofikia wanaliomba kanisa kuleta vielelezo vyao