April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maandalizi ‘Africa Nations Cup’ yapamba moto

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MAANDALIZI ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa Wavu kuelekea kwenye  mashindano ya mpira wa Wavu ya Mataifa ya Afrika ‘Africa Nations Cup’ yatakayoanza kutimua vumbi Septemba 7 hadi 15 nchini Rwanda yamezidi kupamba moto.

Tanzania inashiriki tena mashindano hayo ya mpira wa wavu Mataifa ya Afrika baada ya miaka 44 kwani itakumbukwa kuwa mara ya mwisho walishiriki michuano hiyo mwaka 1977 ilipofanyikia katika nji wa Benghazi nchini Libya.

Mashindano hayo pia yatatumika kwa ajili ya kusaka nafasi ya kushiriki mashindano ya Wavu ya Dunia ‘World Championship 2022’ ambapo kila nchi itawakilishwa na timu ya taifa ya wanawake na wanaume.

Kwa upande wa wanaume, timu zitakazoshiriki ni wenyeji Rwanda, Burundi, Burkina Faso, Cote D’Ivoire, Cameroon, Congo DR, Misri, Ethiopia, Gambia, Guinea, Kenya, Mali, Morocco, Niger, Nigeria, Sudan Kusini, Tanzania, Tunisia, Uganda na Zambia.

Katika kikao kilichofanyika juzi usiku, viongozi wa Chama Cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA) walichagua kikosi cha wachezaji 15 kitakachoongozwa na kocha mkuu, Ally Mohamed kutoka Police Zanzibar akisaidiwa na Nasoro Sharifu wa Jeshi Stars.

Wachezaji waliotwa kwenye kikosi hicho ni pamoja na (Setters) Ezekiel Rabson, Nassoro Mohamed (Jkt), Dismas Dick (Magereza). I Middle Blockers) Ramadhan Mase (Chuff), Abdulhaman Yusuf (Jeshi). Deodatus Baitubaki (Jkt), Michael N’gonge (Jeshi). (Receiver Attackers) David Evarist (Equity Bank, Kenya), Joseph Mafuru (Jeshi), Khantis Sadala (Mafunzo Zanzibar), Ford Edward (Tanesco), (Opposite) Shabani Julius (Chul), Jackson Mmari (Rukinzo Police, Burundi) pamoja na (Liberos) Rashid Mustapha (Jkt) na Said Ali (Mafunzo Zanzibar).

Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA), Alfred Selengia amesema kuwa, wachezaji hao walioweka kambi katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) wanaendelea vizuri na mazoezi yanayofanyika kwenye Uwanja wa ndani wa Taifa ‘Indoor Stadium’.

Amesema, kile kinachooneshwa na wachezaji hao kinaonesha ni namna gani wanapambana kuwa fiti ili kuweza kutimiza mkakati wao kuhakikisha wanawapa matokeo bora na wanapeperusha vema bendera ya Taifa.

Selengia amesema kuwa, kauli iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kuwataka kufanya maandalizi ya kutosha ili kuweza kufanya vizuri imewaongezea morali na watahakikisha wanatanguliza uzalendo ili kuweza kuibuka kimasomaso katika mashindano hayo.

“Kama mnakumbuka Tanzania ilifanikiwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya Afrika kama yale yaliyofanyika katika fukwe za Lido zilizopo Entebbe, Uganda kuanzia Desemba 18 hadi 22, 2019,”.

“Ushindi walioupata Tanzania dhidi ya Uganda, Kenya na Sudan uliwafanya kukaa juu ya msimamo wa kundi lao wakifuatiwa na Kenya ambao nao walifuzu kutinga hatua ya pili huku Sudan wakishika nafasi ya tatu na Uganda wakikaa nafasi ya mwisho na sasa tutahakikisha tunajipanga vizuri ili kuweza kufanya vizuri na ikibidi kufanikiwa kucheza kombe la Dunia,” amesema Selengia.

Kiongozi huyo amesema kuwa, kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka nchini Septemba 5, 2021 chini ya Afisa wa Baraza la Michezo Nchini (BMT) atakaeteuliwa kama mkuu wa msafara.