April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LSF yafanya kikao cha pamoja na ZMOs nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF), limefanya kikao kazi cha pamoja (co-creation meeting) na mashirika (Zonal Mentors Organizations – ZMOs) yatakayosimamia mashirika takribani 92 ya wasaidizi wa kisheria (paralegal organizations) katika kanda sita nchini ili kuongeza ubora, uwezo, na maendeleo ya kitaasisi katika kutoa huduma za msaada wa kisheria katika jamii.

Kikao hicho cha siku mbili kimelenga kupitia maandiko mradi (proposals), mipango kazi (work plans) pamoja na bajeti za mashirika simamizi (ZMOs) kwa ajili ya kuangalia upya shughuli mbalimbali zilizopangwa ikiwa zinaakisi malengo ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki nchini kupitia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho, Meneja Programu LSF, wakili Deogratias Bwire, alisema kuwa kikao kinalenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa watendaji wa mashirika simamizi (ZMOs) kwa ajili ya kuonyesha uelekeo mzuri wa utekelezaji programu ya upatikanaji haki nchini na kuleta matokeo tarajiwa kulingana na miongozo ya LSF ikiwemo mpango mkakati wa miaka mitano pamoja na mpango wa taifa wa maendeleo.

“Kikao hiki kinafanyika ili kukidhi mahitaji ya mabadiliko ya mfumo wa utekelezaji wa programu yetu ya upatikanaji wa haki nchini hasa katika utoaji wa ruzuku.”

Awali, LSF ilikuwa na mfumo wa kutoa ruzuku kwa mashirika ya wasaidizi wa kisheria kupitia mashirika simamizi katika mikoa (Regional Mentors Organizations – RMOs), kisha baadae iliamua kutoa ruzuku moja kwa moja (direct funding modality).

“Sasa tumeamua kuwa na usimamizi wa kikanda ili kuongeza ufanisi zaidi,” ameeleza Meneja Programu.

Meneja wa Usimamizi na Matokeo LSF, Said Chitung alisema kuwa kikao hicho kinalenga kuongeza usimamizi wa programu kwa kujenga uwezo kwa mashirika ya msaada wa kisheria ambayo ZMOs watayasimamia katika kanda zao.

“ZMOs hawa kazi yao kubwa ni kufanya usimamizi wa programu ya LSF katika mikoa mbalimbali ambayo watakwenda kuisimamia kulingana na kanda zao tulizowapa.  Tunategemea mfumo huu utupe matokeo makubwa zaidi mwisho wa programu yetu kama tulivyokubaliana katika kikao hiki muhimu,” alisema Chitung.

Afisa fedha kutoka Shirika la Morogoro Paralegal Centre (MPLC), Regina Solomon alieleza kuwa kikao kimesaidia kujenga uelewa wa pamoja katika utoaji wa taarifa (reporting) zenye matokeo kuhusu utekelezaji wa mradi katika maeneo ambayo ZMOs atakwenda kuyasimamia chini ya ufadhili wa Legal Services Facility.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Centre for Widows and Children Assistance (CWCA), Wakili Jane Kapufi alisema taasisi yake ambayo imechaguliwa kusimamia (ZMO) mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga watahakikisha mashirika ya msaada wa kisheria yanakuwa hai zaidi kiutendaji kwa kuendelea kuyajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria ikiwemo kutoa mafunzo ya sheria ambazo zimekuwa na tabia ya kubadilika kila wakati.

Kikao kazi hicho cha pamoja kimeandaliwa na LSF kwa siku mbili kuanzia Februari 9 hadi 10, 2023 jijini Dar es Salaam, ambapo mashirika simamizi (ZMOs), waratibu wa kanda wa programu na usimamizi wa ruzuku LSF (LSF zonal Coordinators) kwa pamoja watashirikiana na secretarieti ya LSF kujenga uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki kupitia usimamizi wa kanda.

Meneja Programu wa Legal Services Facility (LSF), Wakili Deogratias Bwire